Home Habari YANGA MAMILIONI HAYOO

YANGA MAMILIONI HAYOO

417
0
SHARE

NA JESSCA NANGAWE,

IKIWA ni siku moja tangu uongozi wa Yanga uanze zoezi la ukusanyaji fedha kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo, tayari klabu hiyo imeanza kupokea fedha kutoka kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa soka.

Juzi uongozi wa Yanga ulizindua harambee kwa ajili ya watu mbalimbali kuichangia timu hiyo kifedha ili iweze kuendelea na shughuli zake za kimaendeleo, zoezi ambalo linaonekana kuanza kwa kishindo.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface ‘Mkwasa’, amesema fedha hizo zitakuwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ndani ya timu hiyo, ikiwamo kuwalipa wachezaji wao ambao mpaka sasa wanadai fedha za mwezi uliopita na mwezi huu.

Mkwasa alisema anashukuru sana kwa vile zoezi la uchangishaji kutoka kwa wanachama limekuwa zuri, kwani wenye mapenzi mema na kikosi chao wameanza kujitoa vilivyo.

“Klabu inathamini mtu wa kipato chochote anachotoa na pia tunatanguliza shukrani za dhati na kutambua umuhimu wa kila mmoja katika mchakato huu,” alisema Mkwasa.

Alisema pia uongozi utakuwa ukitoa taarifa ya makusanyo yote yatakayopatikana kutoka kwa wanachama wake kila baada ya wiki moja ili waweze kufahamu mwenendo mzima wa michango yao kwa klabu.

Aidha, Mkwasa alisema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa mwezi mmoja hadi miwili, huku wakitarajia kupata fedha ambazo zitatosha kuwalipa wachezaji pamoja na shughuli nyingine za maendeleo ndani ya klabu hiyo.

Yanga, ambayo kwa sasa ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56, iko katika harakati za kutetea ubingwa wao na wamepata nguvu kubwa baada ya Simba kupokonywa pointi tatu zilizorudi kwa Kagera Sugar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here