Home Habari YANGA MIKONONI MWA WAARABU

YANGA MIKONONI MWA WAARABU

1088
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

DROO ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika inatarajiwa kupangwa leo na kuna kila dalili Yanga wakaangukia kwenye timu ya Kiarabu, lakini hilo lisiwaumize vichwa mashabiki wa wana- Jangwani hao, kwani benchi lao la ufundi linajua nini cha kufanya.

Mbali na Droo hiyo ya michuano ya Klabu Bingwa, pia timu zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho nazo zitajua hatima yao, ikiwamo Azam FC, ambayo nayo huenda ikaangukia mikononi mwa Waarabu, hata kama si katika raundi za awali.

Yanga watashiriki michuano hiyo baada ya msimu uliopita kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Azam FC wakishiriki Kombe la Shirikisho, baada ya kumaliza nafasi ya pili michuano ya FA walipofungwa na wana-Jangwani hao katika mchezo wa fainali.

Awali kwa Tanzania timu ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ni ile iliyokuwa ikimaliza nafasi ya pili Ligi Kuu, lakini baada ya kuja michuano ya FA, mshindi wa kwanza ndiye anayeshiriki, lakini kama Bingwa wa Ligi Kuu anatwaa tena taji la ubingwa wa michuano ya FA, basi mshindi wa pili wa michuano hiyo ndiye anayeiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho, na hicho ndicho kilichotokea kwa Azam FC.

Katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wataanzia hatua ya awali ambapo wanaweza kujikuta wakipangwa na Al-Ahli Tripoli ya nchini Libya na kama ikishindikana hapo wanaweza kukutana na timu nyingine za Kiarabu katika hatua ya makundi kama watapenya.

Katika timu hizo ambazo zipo hatua ya awali, hakuna ambayo ni tishio sana inayoweza kuwalaza macho Wanayanga kama watacheza lile kandanda lao la kitabuni walilolizoea na hata wakipangwa na hao Al-Ahli Tripoli hakuna kitakachoharibika.

Timu ambazo zipo hatua hiyo ya awali ambazo moja kati ya hizo inaweza ikapangwa na Yanga, ukiachana na Waarabu hao wa nchini Libya, ni Wa All Sras ya nchini Ghana, Zanaco ya Zambia, Saint George ya Ethiopia, Township Rollers ya Botswana, Rail Club du Kadiogo ya Burkina Faso, Vital’O ya Burundi pamoja na Gazelle ya Chad.

Nyingine ni 1º de Agosto ya nchini Angola, Ngaya Club ya Comoro, Sony Ela Nguema ya nchini Eguatorial Guinea, FC Mounana ya nchini Gabon, Gambia Ports ya Gambia, Horoya ya Guinea, Tusker ya Kenya, Lioli ya Lesotho pamoja na Barrack Young Controllers ya Liberia.

Timu nyingine ni CNaPS Sports ya Madagascar, AS Port-Louis 2000 ya Mauritius, Ferroviario Beira ya Mozambigue, AS FAN ya Niger, Saint-Pierroise ya Reunion, APR ya Rwanda, US Goree ya Senegal, Cote d’Or ya Seychelles, Royal Leopards ya Swaziland, KCCA ya Uganda,  Zimamoto ya Zanzibar, CAPS United ya Zimbabwe pamoja na wenyewe Yanga.

Kama Yanga watapambana na kufanikiwa kuvuka hatua hiyo ya awali, wanaweza sasa kukutana na timu kama Etoile du Sahel pamoja na Esperance de Tunis zote za Tunisia, Al-Ahly ya Misri au Zamalek.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alishaweka wazi kuwa timu yoyote watakayopangiwa haitatoka salama, kwani anao uzoefu wa kuzifanyia kitu mbaya timu za Kiarabu wakati akiinoa Zesco United ya Zambia.

Lwandamia alisema yeye kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Ufundi, Hans van der Pluijm, wanaweza kuifikisha Yanga mbali katika michuano hiyo na kwamba mashabiki wasiwe na wasiwasi wowote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here