Home Habari YANGA MOTO ULE ULE

YANGA MOTO ULE ULE

392
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana wamefanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huo ulikuwa mchezo wa mwisho wa Robo Fainali na sasa inaungana na Azam FC, Mbao FC na Simba katika hatua ya Nusu Fainali. Droo ya Nusu Fainali inatarajiwa kuchezeshwa leo.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Hans Mabena, aliyesaidiwa na Mohamed Mkono, wote wa Tanga na Arnold Bugado wa Singida, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Mshambuliaji Amis Tambwe aliifungia Yanga bao la kwanza dakika 15 kwa kichwa, baada ya kuunganisha moja kwa moja nyavuni kona ya winga Geoffrey Mwashiuya.

Kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa, naye akawainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 40, baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya beki Mwinyi Hajji.

Winga  Simon Msuva akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 46 kwa shuti kali.

Pamoja na Yanga kumaliza dakika 45 za kwanza wakiongoza 2-0, lakini wapinzani wao nao walionyesha upinzani kwa kosakosa na kama wachezaji wao, Jeremiah Juma na Benjamin Asukile wangekuwa makini, wangeweza kuipatia timu yao mabao.

Yanga jana walimuanzisha kipa wa tatu, Benno Kakolanya, lakini baadaye walimtoa na nafasi yake kuchukuliwa na kipa wa kwanza, Deo Munishi ‘Dida.’

Dakika ya 55 Tanzania Prisons walipata penalti baada ya Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumchezea rafu eneo la hatari Meshack Suleiman. Lakini penalti hiyo iliyopigwa na Victor Hangai ilidakwa na kipa Dida.

Kikosi cha Yanga: Beno Kakolanya/Deo Munishi ‘Dida’ Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa/Emmanuel Martin, Amis Tambwe/Matheo Anthony na Geoffrey Mwashiuya.

Prisons: Andrew Ntala/Aaron Kalambo, Benjamin Asukile, Salum Kimenya, Leonsi Mutalewa, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhili, Freddy Chudu/Meshack Suleiman, Jeremiah Juma/Victor Hangai, Lambarti Sabiyanka na Mohammed Samatta.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here