Home Habari YANGA SASA HAWATAKI UTANI

YANGA SASA HAWATAKI UTANI

1039
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufungwa kesho, Yanga wanaweza wakafanya usajili wa kushtukiza kwa kushusha mtambo wa mabao, Winston Kalengo, huku Obrey Chirwa akiwekewa mstari mwekundu.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zinadai kuwa, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, George Lwandamina, hajaridhishwa na uwezo alionao Chirwa na sasa anataka kumchinjia baharini na kumleta Kalengo, ambaye hana masihara anapolikaribia lango la timu pinzani.

Chirwa, ambaye alisajiliwa na Yanga kutoka FC Platinum ya Zimbabwe kwa gharama kubwa, ameshindwa kuonyesha kile ambacho mashabiki walikitarajia ambapo taarifa zinadai kuwa, Yanga wanataka kumtoa kwa mkopo katika timu yake hiyo ya zamani.

Taarifa hizo zinadai kuwa, Yanga walishaanza mazungumzo na FC Platinum ili kumchukua Chirwa kwa mkopo, lakini tatizo ambalo limejitokeza ni kwamba, timu hiyo inataka Wanajangwani hao waendelee kumlipa mshahara akiwa huko, kitu ambacho kinaleta ugumu.

“Mipango hiyo ipo, sema tatizo jamaa (Platinum) wanataka akiwa kwao kwa mkopo sisi (Yanga) tuendelee kumlipa mshahara wote, kitu ambacho tunaona siyo sahihi, kwani tumewaambia wao wamlipe nusu nasi tutamlipa nusu, ila wameendelea kushikilia msimamo wao.

“Kama tutaafikiana hilo naamini kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa tutamshusha Winston Kalengo kutoka AC Leopards ya Congo na Obrey Chirwa itabidi arudi kwanza timu yake ya Platinum, hiyo ndiyo mipango yetu na kama ikishindikana tutajua hapo,” alisema kigogo mmoja wa Yanga.

Unaweza ukajiuliza, Winston Kalengo ni nani? Huyu ni mshambuliaji anayeichezea AC Leopards ya nchini Congo, aliyezaliwa mwaka 1985 katika mji wa Livingston, nchini Zambia ambapo mpaka sasa amefikisha miaka 31.

Jina lake lilianza kuwika msimu wa mwaka 2004-2011, alipokuwa akiichezea Zanaco FC ya nchini humo, ambapo aliifungia jumla ya mabao 52, kabla ya kusajiliwa na Zesco msimu wa mwaka 2011-12, akifunga mabao nane na baadaye aliamua kurudi kwenye timu yake ya Zanaco F.C msimu wa 2012, ambapo aliifungia mabao matano.

Hakuweza kukaa sana katika kikosi hicho cha Zanaco FC, kwani uwezo aliouonyesha uliwashawishi Zesco United kumrudia tena ambapo alicheza kuanzia msimu wa mwaka 2013-15 na kuonyesha uwezo mkubwa, akifunga jumla ya mabao 38, kabla ya kuhamia AC Leopards ya Congo ambapo taarifa nyingine zinadai kuwa Zesco wanammezea mate tena na sasa watapambana na Yanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here