Home Habari YANGA, SIMBA NA SOKA LA MAZOEA

YANGA, SIMBA NA SOKA LA MAZOEA

7645
0
SHARE

NN KAKA MWINYI

KATIKA maisha hakuna kitu muhimu kama tumaini. Kwa tafsiri halisi ya neno hilo ni aina ya subira inayomhusisha kila mwanadamu mwenye akili timamu kutokana na kile akifanyacho bila kujali ni kazi, shughuli, kilimo, biashara, michezo au sanaa. Lakini ndani ya tumaini kuna ziada ya bidii na uwajibikaji kwa ufanyacho ili kupata matokeo chanya.

Msingi wa utangulizi huo umechagizwa na mtindo wa klabu mbili kubwa na kongwe hapa nchini (Yanga na Simba), ambazo mbali ya kuwa na mitaji mikubwa ya wapenzi, wanachama na mashabiki, bado zimekuwa zikisuasua katika safari ya kuyaelekea mafanikio ya kweli ambayo kila mmoja ndani yake anayatamani kama si kuyataraji.

Klabu hizi kila zinavyojaribu kujiinua kwa kasi ya kobe kutoka zilipo, zimeendelea kuwa mifano isiyofaa kwa klabu ndogo au changa za mchezo wa soka kutokana na kukosa dira sahihi zitakazoziwezesha kujikwamua na kujiweka kwenye viwango vya kimataifa, kwa kuzilinganisha na klabu nyingine maarufu za soka barani Afrika na Ulaya.

Tatizo kubwa linalozikabili klabu hizi ni kuendesha mambo yake kwa mazoea. Kuanzia utendaji wa uongozi, walimu, wachezaji na hata wadhamini (wafadhili) wake, kila kukicha wamekuwa hawana jawabu jipya au njia mbadala za kuhakikisha zinabadilika na kufikia malengo zilizojiwekea. Daima zimetawaliwa na uendeshaji wa ki-mazoea zaidi.

Si ajabu kuona au kusikia wanaowania nafasi za uongozi wa uendeshaji wa klabu hizi wakijinadi hadharani kwa kutaja mikakati na mbinu zinazowashawishi wapiga kura kuwapa ‘ulaji’ kwa matamanio ya kupata kilicho bora, lakini kinyume chake mara baada ya kukabidhiwa ofisi mambo yote hubaki yaleyale kiasi cha kuwafanya wenye kutafakari kushindwa kubainisha tofauti ya viongozi waliotoka na walioingia. Hii imekuwa kasumba inayoelekea kukosa dawa kama si tiba kabisa.

Timu hizi mbili ndizo zimenilazimisha kuandika makala haya kwa kuzingatia vigezo vingi tu vilivyo bayana. Ukongwe, uzoefu wa ushiriki wa ligi na michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, ‘utajiri’ wa mashabiki kulinganisha na kilabu kama Azam, Coastal Union, Mbeya City, Mbao FC na nyingine, zimeshindwa kabisa kuonesha mwanga au kufungua milango kwa kilabu zilizo nyuma yao.

Bado najiuliza huku nikikosa majibu ya moja kwa moja, ni nini hasa tatizo la msingi linalozikabili klabu hizi. Sijui ni uongozi usioweza kusimamia majukumu yake?! Sijui ni mifumo ya kiuendeshaji kutoka kwa walimu? Yaani sijui. Labda ni mfumo wa Serikali kupitia baraza lenye dhima ya kusimamia michezo kukosa mipango yenye tija kwa soka letu?! Bado sielewi hasa ni wapi klabu hizi zinakosea ili kujiimarisha na kuwa mifano kwa zile ndogo.

Si kwamba ninazisimanga Yanga na Simba, la hasha. Najaribu kueleza kilicho ndani ya akili za wapenzi na washabiki wengi wa soka la Tanzania ambao mara kwa mara wamekuwa wakipishana kutoa maelezo yao yaliyozama kwenye lawama kwa kutofanikiwa kwa soka letu. Mifano iko tele katika mahojiano ya wapenzi na wadau wa soka kila uchao kuonesha kutoridhishwa na maendeleo ya klabu hizo kwa ujumla.

Binafsi, kwa kutumia rasilimali watu zilizo nazo, Yanga na Simba zingeshakuwa vinara wa soka katika ukanda huu wa Mashariki mwa Afrika kutokana na ukweli kwamba, Watanzania ndio wanaoongoza kwa upenzi na ushabiki wa soka Afrika Mashariki. Cha kushangaza, ki-viwango hasa vile vya FIFA, sisi ndio tumekuwa tukiishia nafasi ya tatu au nne baada ya Uganda na Kenya. Sitashangaa nikisikia Rwanda wako juu yetu kwa viwango vya soka.

Kwa mantiki hiyo, napenda kuzishauri kilabu hizi kupitia viongozi wake kuhakikisha zinaweka mikakati ya dhati itakayoziwezesha kupanda ngazi hatua kwa hatua kuyafuata mafanikio. Ziachane na mawazo ya kufanya kazi kwa mazoea kwani mwisho wa yote ni kupata matokeo yasiyo na faida kimataifa bali kitaifa pekee, kwani huishia kusababisha tambo, kejeli na majivuno baina ya wapenzi wa klabu hizo.

Kumekucha, amkeni, chapeni kazi kwa dhamira ya kuwa wa mifano iliyofanikiwa si iliyodidimia. Kumbukeni ninyi ndio vioo kwa klabu ndogo na hata zile mpya kwa hiyo msitoe taswira isiyopendeza kwa wanaowaangalia. Jitambueni na jiulizeni nini na kipi cha kufanya kabla hamjawa wa kimataifa kwa maana halisi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu libariki soka letu.

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here