Home Habari YANGA: STAND, SIMBA WOTE WATAACHIA TU

YANGA: STAND, SIMBA WOTE WATAACHIA TU

1409
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

YANGA wamesikia kwamba wenzao Simba wameibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji, na sasa wamejipanga kuhakikisha wanaishushia kipigo kizito Stand United leo na pia kwenda kuwawinda watani zao hao wa jadi wiki ijayo, ili kuwakata kilimilimi.

Simba waliibuka na ushindi wa mabao hayo na kuzidi kujichimbia kileleni wakifikisha jumla ya pointi 15, na kama Yanga ambao wanazo pointi 12 watashinda leo, watalingana na watani zao hao wa jadi, ambapo timu hizo zitakuwa zikizidiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na lengo moja tu, kushinda na baada ya hapo kwenda kujichimbia kwa ajili ya kuwawinda Simba Oktoba 28, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ameliambia DIMBA kwamba, licha ya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kutaka kushinda uwanja wao wa nyumbani, amewaandaa vijana wake kuondoka na pointi zote tatu.

Licha ya kwamba Lwandamina atawakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu, akiwamo Thaban Kamusoko, Donald Ngoma pamoja na Amis Tambwe, kutokana na majeraha yanayowakabili, wana uhakika wa kushinda.

Uhakika wa ushindi kwa Wanayanga unatokana na ukweli kwamba, tangu Stand United kuanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, 2014/15, ikitoka Ligi Daraja la kwanza, imecheza michezo sita dhidi ya Yanga, ikishinda mmoja tu, mingine mitano ikiambulia vipigo vya maana.

Mchezo huo ambao Stand United, walishinda ulikuwa ni wa msimu uliopita, ukichezwa Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga na wenyeji hao kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Walipopanda daraja msimu wao wa kwanza 2014/15, michezo yote miwili walifungwa, wakianza kukubali kichapo cha mabao 3-0, Oktoba 25, 2014, Uwanja wao wa nyumbani wa Kambarage, kabla ya kufungwa tena mabao 3-2, Uwanja wa Taifa mzunguko wa pili Aprili 21, 2015.

Msimu uliofuata, yaani 2015/16, hali haikuwa nzuri tena kwa Stand United, kwani mchezo wa mzunguko wa kwanza walikubali kichapo cha mabao 4-0, Uwanja wa Taifa, Desemba 19, 2015, na baadaye kufungwa tena mabao 3-1, Uwanja wao wa Kambarage, Mei 3, 2016.

Msimu uliopita angalau ndio walijitutumua na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Uwanja wao wa Kambarage, Septemba 25, 2016, na baadaye kufungwa mabao 4-0, Uwanja wa Taifa, mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Februari 3, 2017.

Hata hivyo, licha ya rekodi hiyo nzuri ya Yanga, kocha wa Stand United, Athuman Bilal, amesema leo watahakikisha wanawatoa nishai mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuwafunga mabao ya kutosha.

“Utakuwa mchezo mgumu, lakini naamini tutaondoka na pointi tatu, kwani hata msimu uliopita tulipokutana nao Uwanja wetu huu wa nyumbani tuliwafunga bao 1-0, hivyo hatuna wasiwasi wowote na badala yake dakika 90 ndizo zitakazotoa mbabe,” alisema.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na ukweli kwamba, kila timu inataka kupata matokeo mazuri, ili kujiweka kwenye nafasi nzuri, hasa Stand United, kwani katika michezo sita waliyocheza wameshinda mmoja tu, wakifungwa minne na kutoka sare mmoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here