Home Habari YANGA: UBINGWA UPO PALEPALE

YANGA: UBINGWA UPO PALEPALE

682
0
SHARE

NA JESSCA NANGAWE,

WAKATI mashabiki wa Simba wakitembea kifua mbele wakidai kuwa ubingwa msimu huu ni wao, hasa baada ya kuwafunga Yanga, Wanajangwani hao wamejibu mapigo wakidai kuwa, hakuna wa kuwapokonya ubingwa wao.

Katika mchezo uliozikutanisha timu hizo mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, kitu ambacho kinawapa jeuri ya kusema watatwaa ubingwa msimu huu, lakini Yanga wenyewe wameibuka na kusema watani zao hao wa jadi wanaota ndoto za mchana.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, wanaoamini kuwa mbio zao za ubingwa zimeishia pale walipofungwa na Simba, wanajidanganya, kwani wao wanachoamini ni kwamba watashinda michezo yao yote iliyobakia na kwamba watatetea ubingwa wao.

“Si kweli kwamba hatupo kwenye mbio za ubingwa, nadhani wanaosema hivyo wanapotosha, kwani kufungwa na Simba hakumaanishi kwamba tutarudi nyuma.

“Tunachoamini ni kwamba, sisi kama mabingwa watetezi tunayo nafasi ya kuutetea ubingwa wetu na hilo linawezekana, kwani bado Ligi inaendelea na pointi ambazo tumeachana na waliopo kileleni sio nyingi, ikizingatiwa kuwa tunao mchezo mmoja wa kiporo,” alisema.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanashuka leo uwanjani kucheza na maafande wa Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo Mwambusi amesema watashusha silaha zao zote kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu.

“Kwanza niseme si mchezo rahisi, kwani hata wapinzani wetu wamejiandaa kuondoka na pointi tatu, lakini nikwambie tu kwamba mashabiki wetu hawatakiwi kuogopa chochote, kwani tumefanya maandalizi mazuri.

“Tunachotaka kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda michezo yetu iliyosalia, hatuna muda wa kuendelea kufikiria matokeo yaliyopita, kikubwa sasa ni kuweka akili zetu katika mechi zilizobaki na kuhakikisha tunapigana kufa na kupona ili tuweze kushinda,” alisema Mwambusi.

Aliongeza kuwa, wachezaji wote wapo katika hali nzuri, isipokuwa straika wao, Donald Ngoma, ambaye bado hali yake haijawa nzuri, japo inaendelea kuimarika na siku si nyingi atarejea uwanjani.

Katika msimamo wa ligi Wanajangwani hao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 49, ambapo kama watashinda leo watafikisha pointi 52, wakizidiwa na Simba kwa pointi mbili,  kwani wekundu hao wa Msimbazi wana pointi 54.

Hata hivyo, mchezo huo unaweza usiwe rahisi sana kwa Yanga, kwani wakati wenyewe wakijitapa kwamba watashinda, Ruvu Shooting nao wamekuja juu, wakisema iwe mvua au jua, lazima waondoke na pointi zote tatu.

Msemaji wa maafande hao, Masau Bwire, alisema: “Hawa Yanga ni sawa na kumsukuma mlevi, kwani Simba walishamaliza kazi walipowafunga mabao 2-1 na sisi tunakwenda uwanjani kumalizia tu kazi”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here