Home Habari YANGA VS AZAM NI VISASI TUPU

YANGA VS AZAM NI VISASI TUPU

506
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea tena leo Jumapili kwa mechi nne kupigwa katika viwanja tofauti tofauti lakini akili za wengi hazitakuwa huko badala yake nchi itasimama kidogo na Jiji la Dar es Salaam litahamia Uwanja wa Uhuru kushuhudia mchezo wa kumaliza ubishi kati ya Yanga na Azam.

Yanga na Azam zinakutana kwa mara ya kwanza katika ligi msimu huu tangu zilipokutana mara ya mwisho miezi miwili iliyopita katika mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 17 mwaka huu, Yanga ikafa kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 katika dakika 90.

Tofauti na mechi nyingi, mechi ya leo itakuwa kali na yenye msisimko mkubwa kutokana na ukweli kwamba Yanga watataka kuwafukuzia mahasimu wao Simba kileleni, huku Azam wao wakitaka kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi baada ya kuteleza hivi karibuni.

Yanga watataka kushinda mchezo huo ili kudhihirisha kuwa hawakupata ubingwa msimu uliopita kwa bahati mbaya huku Azam nao wakitaka kushinda ili kuwaonyesha Wanajangwani hao kuwa bado wana ubavu.

Wanajangwani hao wanaingia katika mchezo huo wakiwa wamecheza michezo saba wakishinda minne, wametoka sare michezo miwili na kupoteza mmoja dhidi ya Stand United, hivyo kujikusanyia pointi 14.

Kwa upande wao Azam FC wamecheza michezo nane wakifanikiwa kushinda mitatu tu na wametoka sare michezo miwili, huku wakipoteza michezo mitatu na kujikusanyia pointi 11.

Timu hizo zinakutana huku makocha wa pande zote mbili wakiwa na presha ya kulinda vibarua vyao, ambapo kwa upande wa Yanga taarifa zinadai kuwa nafasi ya Hans Van De Pluijm, iko mashakani kwani iwapo atapoteza mchezo wa leo huenda akaondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Azam FC raia wa Hispania, Zeben Hernandez, amekalia kuti kavu kutokana na kikosi chake kushindwa kupata matokeo mazuri kama ilivyozoeleka hivyo naye yupo kwenye mstari mwekundu.

Kutokana na hali hiyo, kila kocha anatarajiwa kupanga kikosi cha maangamizi ili kuhakikisha anaondoka na pointi zote tatu hali ambayo itaufanya mchezo wa leo kuwa mkali kwa dakika zote 90.

Katika mchezo wa leo Yanga itamkosa mshambuliaji wake tegemeo, Amissi Tambwe ambaye alipata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar lakini hiyo haiwatii hofu mashabiki wa Wanajangwani hao kutokana na uwepo wa Donald Ngoma, huku Obrey Chirwa naye akiwa ameshaanza kufufuka.

Jambo la kufurahisha katika timu hizi ni kwamba ni kama zimelingana kila kitu kwani zimekutana mara 16 katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Yanga wameshinda mara tano na Azam wakashinda mara tano huku zikitoka sare mara sita na kila moja imemfunga mwenzake mabao 25.

Msimu uliopita timu hizi zilipokutana mchezo wa mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, zikatoka tena sare ya kufungana mabao 2-2 mzunguko wa pili ambapo leo ndipo itajulikana nani mkali zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here