Home Habari YANGA VS NDANDA, Afe kipa, afe beki

YANGA VS NDANDA, Afe kipa, afe beki

706
0
SHARE


EZEKIEL TENDWA NA ZAINAB IDDY

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, wanajua kuwa mara ya mwisho kuchezea Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara walikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC na sasa wamekoki bunduki zao kuhakikisha wanafuta uteja huo leo, katika mechi ambayo inatarajiwa kuwa ya ‘kufa mtu.’

Wanajangwani hao jana walisafiri kwa basi kuelekea mjini Mtwara na kupata mapokezi makubwa kabla ya kufikia katika hoteli ya kifahari ya Tiffany, mjini humo. Wameapa kwamba kwa vyovyote vile leo, afe kipa, afe beki, ni lazima wapate ushindi ili kuendeleza kampeni yao ya kuutetea ubingwa wao walioutwaa msimu uliopita.

Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakuwa wageni wa Ndanda FC mchezo wa Ligi ambao utachezwa kwenye Uwanja huo leo, huku Wanajangwani hao wakiwa na nia moja tu ya kushinda.

Timu hizi zinapokutana mchezo huwa mkali kwa dakika zote 90 ambazo katika msimu wa 2014/15 ambao ndiyo Ndanda FC walipanda daraja, waliweza kuwafunga Yanga bao 1-0 kwenye uwanja huo wa Nangwanda, katika mchezo wa mzunguko wa pili.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huo, timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0, mchezo ukichezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya ushindi huo walioupata Ndanda mzunguko wa pili mkoani Mtwara.

Msimu uliopita Yanga waliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0, mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 Uwanja huo wa Taifa, baada ya Wanajangwani kuomba mchezo wao huo uchezwe hapo ili kukabidhiwa kombe lao.

Hesabu zinaonyesha kuwa matokeo ya misimu hiyo miwili hakuna mbabe, kwani licha ya Yanga kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Nangwanda, walilipiza kwa ushindi kama huo Uwanja wa Taifa, lakini sasa Wanajangwani hao wanataka kuonyesha kwamba wao ndiyo baba wa soka la bongo watakapowakabili wapinzani wao hao leo.

Yanga wanajua kuwa wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kutetea ubingwa wao kutokana na wapinzani wao wa jadi, Simba, kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafuta uteja wa misimu minne mfululizo bila kutwaa ubingwa huo wa Ligi Kuu.

Katika kuhakikisha wanatetea ubingwa wao, Wanajangwani hao wamekuwa wakijifua vilivyo katika viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuondoka jana asubuhi kuelekea mkoani Mtwara kwa ajili ya mcheo huo wa leo.

Kwenye mechi ya leo dhidi ya Ndanda ambao hadi sasa wamecheza mechi 2 za ligi na kufungwa zote na Simba na Mtibwa Sugar, Yanga itawakosa wachezaji wao kadhaa.

Kikosi cha Yanga cha wachezaji 20 chini ya Kocha Hans van Pluijm kilichosafiri kwa basi kwenda Mtwara kitawakosa nyota wake sita, akiwemo kipa namba moja, Deogratius Munishi ‘Dida’, aliyefiwa na baba yake mzazi na majeruhi Pato Ngonyani, Malimi Busungu na Geofrey Mwashiuya.

Wengine ambao hawamo kikosini ni mapro wao Vincent Bossou aliyekuwa na timu ya Taifa ya Togo na Haruna Niyonzima, aliyekuwa na timu ya taifa ya Rwanda kushiriki mechi za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon na bado kurejea.

Akizunguzia mchezo huo, Pluijm alisema licha ya kwamba utakuwa mgumu kutokana na kila timu kujipanga, ana imani kuwa kikosi chake kitaibuka na ushindi mnono.

“Hakuna mchezo rahisi hata kidogo, kila timu imejiwekea mikakati yake ya kuhakikisha inashinda, ndiyo maana kamwe siwezi kuidharau timu yoyote, tutaingia kwa nguvu zetu zote ili tuondoke na pointi tatu, maana hizo ni muhimu sana kwetu kama mabingwa watetezi,” alisema.

Katika mchezo wao wa ufunguzi, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, mabao yakifungwa na Deus Kaseke, Juma Mahadhi pamoja na Simon Msuva.

Kwa upande wao Ndanda FC, wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo yao miwili iliyopita na sasa watataka kuibana Yanga ili angalau wajizolee pointi, kitu ambacho Yanga wenyewe hawawezi kukubali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here