SHARE

NA MAREGES NYAMAKA


MABINGWA wa kihistoria nchini, Yanga, wanaendelea kujifua Mji Kasoro Bahari, mkoani Morogoro kwa ajili msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, chini ya kocha kutoka DRC, Zahera Mwinyi.

Maandalizi hayo yana maingizo mapya yaliyosajiliwa msimu huu, huku yakiwafanya mashabiki wengi kukosa imani nayo.

Kiashiria cha kukosa tabasamu kwa wana Yanga, ni maneno yanayosikika  vinywani mwao yakieleza bayana kutokuwa na imani na usajili wa aina hiyo ambao katika klabu hiyo hawajauzoea.

Sura mpya ndani ya kikosi hicho  iliyofanywa na Kamati ya Usajili  kupitia kwa Mwenyekiti wake, Hussein Nyika, ni wachezaji Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mohamed Japhary, Mohamed Issa, Klaus Kindoki na Heriter Makambo kutoka nchini DRC.

Kilichofanywa na Nyika ni sawa na mbuzi kula kulingana na urefu wa kamba yake, maana kuna ukweli kwamba klabu haikuwa vizuri kimapato.

Ni ngumu kukikimbaza na timu kama za Singida United, Simba na Azam ambao wanaonekana wako vizuri katika eneo hilo la uchumi, lakini pia ushirikiano ukiwa wa hali ya juu sana.

Katika usajili huo wa Yanga ukijimuisha na wachezaji waliosalia,  unaiona kazi kubwa ya kocha Zahera ambaye atalazimika kuipanga vizuri timu yake hasa nafasi ya ulinzi ambako hakukuwa na ingizo jipya.

Pia kulikuwa na mapungufu baada ya beki wake wa kulia, Hassan Kessy kutimkia Zambia ambako inaelezwa amejiunga na timu ya Nkana Red Delvis.

Kwa maana hiyo, nafasi hizo sasa zitakuwa chini ya Juma Abdul, Pato Ngonyani, Andrew Vicent ‘Dante’ Abdlalah Shaib wote hao wakitegemea uzoefu wa Kelvin Yondani ambaye ni kiongozi wa eneo hilo.

Yondani alipokosekana katika michezo kadhaa ikiwamo mechi tano alizofungiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), hakukuwa na muunganiko eneo hilo, hiyo inaleta mashaka katika michuano ijayo ya ligi yenye jumla ya timu 20 msimu huu.

Hata hivyo, inawezekana kocha huyo naye akaibuka na hatua zake pengine akafanya ‘surprise’ kwa kumtumia mchezaji mwingine badala ya Yondani kama zilivyo falsafa za makocha wengi.

Kwa upande wa ushambuliaji, zinahitajika juhudi za kuficha pengo la mpachika mabao, Obrey Chirwa, kazi ambayo rasmi inatakiwa kufanywa na mrithi wake Mcongo, Makambo ambaye ni pendekezo la Zahera mwenyewe.

Pembeni ya Mcongo huyo yupo Ibrahim Ajib ambaye licha ya uwezo mkubwa alionao, lakini inabidi kuangaliwa zaidi kutokana na mabadiliko yake yasiyotarajiwa.

Katika safu ya kiungo, hapo kwanza ndipo hakuna mchezaji aliyeondoka, kikubwa zaidi wameongezwa watu wengine wa kazi, maana yake upinzani wa nafasi unakuwa mkubwa.

Chipukizi Fei Toto ambaye amecheza mashindano kadhaa makubwa ikiwamo Ligi ya Mabingwa (Afrika Caf), akiwa na JKU ya Zanzibar, ana nafasi kubwa ya kuwania namba ndani ya kikosi cha kwanza, licha ya eneo hilo kuwepo akina Papy Kabamba Tshishimbi, Thaban Kamusoko, Thaban Kamusoko, Jafary Mohammed, Mohammed Issa ‘Banka’ na  Raphael Daud.

Inaweza kuwa Yanga itakayotisha endapo ndoto ya kocha Zahera itakwenda sawia na aina ya wachezaji alionao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here