SHARE

NA MWAMVITA MTANDA 

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuingia dimbani Ijumaa hii kuvaana na Alliance FC ya jijini Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kuelekea mchezo huo, Yanga itakuwa na ukuta kamili wakiwemo mabeki wake ambao wamezikosa mechi kadhaa kama vile Lamine Moro ambaye alikuwa majeruhi na Kelvin Yondani aliyekuwa na kikosi cha timu ya taifa.

Wanajangwani hao wanaondoka leo na jumla ya wachezaji 18 pamoja na benchi zima la ufundi likiongozwa na kocha mkuu, Charles Boniface Mkwasa.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 13, wakati Alliance ipo nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi 17.

Akizungumza na DIMBA Jumatano jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema maandalizi yao yamekamilika na wapo tayari kwenda kuzitafuta pointi tatu kutoka kwa Alliance.

Alisema wachezaji wote watakaosafiri wako fiti isipokuwa wawili ambao ni majeruhi ambao ni Maybin Kalengo na Issa Bigirimana.

“Tumeamua kupambana vilivyo msimu huu, mipango ya kocha Mkwassa ni kuhakikisha tunashinda kila mechi ili tujiweka vizuri katika msimamo wa ligi,” alisema Mwakalebela.

Yanga ilionekana kupawaya katika nafasi ya ulinzi wakati ilipocheza na JKT Tanzania licha ya kushinda mabao 3-2 na Mwakalebela anasema safari hii mabeki wao tegemeo ambao hawakuwepo kikosini nao watakuwa sehemu ya mchezo huo.

Kikosi hicho kiliingia uwanjani huku beki wake Lamine Moro akionekana kuwa majeruhi na vilevile Kelvin Yondani alikuwa akikitumikia kikosi cha timu ya taifa.

“Mabeki wetu wote wataondoka, kwa upande wa Lamine aliyecheza chini ya kiwango wakati wa mechi yetu na JKT Tanzania, sasa yuko fiti vilevile Yondani aliyekuwa Taifa Stars naye yumo kikosini,” alisema.

Mwakalebela alisema tayari wameshafanya mawasiliano na wanachama pamoja na wadau wa Yanga waliopo Mwanza kwa ajili ya kuipokea timu yao na kuipa sapoti wakati wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Timu ya Yanga imekuwa ikipata mapokezi makubwa katika jiji la Mwanza na mara ya mwisho wanachama wao waliialika timu yao na kufanya harambe ya kuichangia wakati ilipokuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here