Home Habari YANGA YAFANYA MAAMUZI MAGUMU

YANGA YAFANYA MAAMUZI MAGUMU

443
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

BAADA ya Yanga kumruhusu kiungo wake Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, kuondoka kutokana na kutaja dau kubwa, baadhi ya wachezaji nyota nao wameanza kudengua, wakitaka mkwanja wa maana ndipo waongeze mikataba yao, na sasa uongozi wa Wanajangwani hao umeamua kuchukua maamuzi magumu.

Moja ya maamuzi ambayo uongozi huo umefikia ni kwa wale wachezaji wote ambao wataonyesha usumbufu wowote kuonyeshwa mlango wa kutokea, ili wasajiliwe wengine watakaoonyesha mapenzi mema na timu.

Uongozi umeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuenea taarifa kwamba, straika wao Mzimbabwe, Donald Ngoma, anataka kuongeza mkataba kwa fedha nyingi ambazo kwa vyovyote zinaweza zikawashinda Wanajangwani hao.

Mbali na Ngoma, taarifa nyingine zinadai kuwa, hata kiungo Mzimbabwe mwingine, Thaban Kamusoko, naye amewaambia kama wanataka kumbakisha mitaa hiyo ya Twiga na Jangwani, watatakiwa kuweka mezani kitita cha Dola za Kimarekani 60,000, ambazo ni zaidi ya Sh milioni 130 za Kitanzania.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia DIMBA kwamba, hawatakuwa radhi kutoa fedha nyingi kwa mchezaji mmoja na kwamba atakayetaka kuondoka watamruhusu kwa moyo mweupe, kwani hawawezi kujilazimisha kufanya kitu ambacho kitawaletea matatizo mbele ya safari.

“Haruna (Niyonzima) tumeamua kuachana naye baada ya kutaja dau kubwa, sasa akitokea mwingine naye akataka kama mwenzao alivyotaka nadhani hatutawezana naye na badala yake tutamwonyesha mlango wa kutokea.

“Sisi hatuwezi kulazimisha kitu ambacho kitatuletea matatizo mbele ya safari, kwa sasa tunaendelea kufanya mazungumzo na Ngoma na Kamusoko na wameonyesha dalili za kukubaliana na kile tulichonacho, lakini kama nao wakisema wanataka kikubwa zaidi, nadhani tunaweza tukafanya kama ilivyokuwa kwa Haruna,” alisema kigogo huyo.

Kigogo huyo alisema wachezaji hao kutoka Zimbabwe, wanatarajiwa kutua nchini ndani ya wiki inayoanza kesho, ambapo DIMBA lilipomuuliza kuhusu tetesi za kwamba Ngoma anawindwa na Simba, alisema taarifa hizo hawana na badala yake anaamini kwamba wataendelea kumtumia msimu ujao, kwani mazungumzo yao yanakwenda vizuri.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here