Home Habari YANGA YAFANYA MAUAJI GEITA

YANGA YAFANYA MAUAJI GEITA

440
0
SHARE

NA SALMA MPELI,

YANGA imemalizia hasira za kutolewa kwenye michuano ya Kombe la FA dhidi ya Mbao, kwa kufanya mauaji mkoani Geita, ambapo jana iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya timu ya Buseresere ya Geita.

Yanga iling’olewa na Mbao mwishoni mwa wiki katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA, iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na hivyo kujikuta ikivuliwa ubingwa.

Baada ya kutoka mkoani humo, kikosi cha Wanajangwani hao kiliamua kuweka kambi ya siku mbili Geita, ambapo jana ilicheza mchezo huo wa kirafiki wa kujiweka sawa uliopigwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Geita.

Hadi mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na Deus Kaseke dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza na baada ya kurejea kipindi cha pili, Emanuel Martin aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 48.

Martin aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea JKU ya Zanzibar, aliwainua tena mashabiki wa timu hiyo dakika ya 73 akifunga bao lake la pili kwenye mchezo huo na la tatu kwa timu yake.

Matheo Antony aliongeza bao la nne katika dakika ya 89 kabla ya kumalizia karamu ya mabao ya Yanga  dakika ya 90 ya mchezo na kuifanya timu yake kutoka kifua mbele kwa ushindi huo mnono.

Timu hiyo inatarajiwa kurejea jijini kesho kwa ajili ya maandalizi yake ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here