Home Habari YANGA YAFANYIWA KITU MBAYA ALGERIA

YANGA YAFANYIWA KITU MBAYA ALGERIA

295
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU, ALGIERS

YANGA wametupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la soka Barani Afrika kwa jumla ya mabao 4-1 kufatia kipigo cha magoli 3-0 ugenini dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Mchezo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga walipata ushindi mwembamba wa goli 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezeshwa mwamuzi Yakhouba Keita, akisaidiana na Aboubacar Doumbouya na Mamady Tere wote kutoka Guinea, hadi mapumziko Yanga walikuwa nyuma kwa mabao 2-0, kwa mabao ya Sid Ahmed Aouedj na Walid Derrardja.

Wenyeji walionekana kupania vilivyo tangu dakika ya kwanza wakicheza soka la kujiamini la pasi ndefu na fupi huku wakipeleka mashambulizi ya kushtukiza.

Baada ya mashambulizi ya dakika 15, MC Alger walifanikiwa kuandika bao la kwanza kupitia kwa Aouedj, ambaye aliukwamisha wavuni mpira baada ya piga nikupige langoni mwa Yanga.

Ulianza mpira wa kona ambayo iliokolewa kizembe na mabeki wa Yanga na ndipo mpira ukamkuta mfungaji aliyeutupia wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliwachanganya kiasi Yanga ambapo mabeki wake Kelvin Yondani na Nadir Haroub Cannavaro walionekana kutofautiana hali iliyowafanya Waalgeria kuzidi kuwashambulia na kufanikiwa kupata bao la pili.

Bao hilo lilitokana na mpira wa adhabu, baada ya Cannavaro kumchezea rafu mshambuliaji wa MC Alger, na ndipo mwamuzi akaamuru upigwe mpira wa adhabu ambao uliwekwa kimiani na Derrardja kwa shuti la moja kwa moja lililomshinda kipa wa Yanga Deogratias Munishi ‘Dida’.

Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa kufanya mabadiliko ambapo alimtoa Deus Kaseke na kumwingiza Amis Tambwe, Andrew Vicent akachukua nafasi ya Cannavaro na Geofrey Mwashiuya akamrithi Donald Ngoma.

Mabadiliko hayo hata hivyo hayakuwasaidia Yanga kwani waliweza kuongezwa mabao mengine mawili kipindi hicho ambapo Zahir Zerdab alifunga dakika ya 70 na Aouedj akamalizia bao la nne ambalo ni la kwake la pili kwa siku ya jana.

Kwa matokeo hayo Yanga inaonyesha kwamba bado haijapata dawa ya Waarabu kwa kipindi cha miaka 35, iliyokutana nao.

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga haijawahi kuitoa kwenye mashindano ya klabu Afrika timu yoyote kutoka Uarabuni.

 1. Yanga 1-6 Al Ahly-1982

Mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilikung’utwa 5-0 nchini Misri, kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 6-1 mwaka 1982.

 1. Yanga 0-4 Al Ahly-1988

Mwaka 1988, Yanga ilicheza mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa mara nyingine na Al Ahly na katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, timu hizo hazikufungana, kabla ya Yanga kulala 4-0 ugenini.

 1. Yanga 1-2 Ismailia-1992

Yanga ilicheza tena Ligi ya Mabingwa ikiwa ni raundi ya kwanza dhidi ya Ismailia ya Misri mwaka 1992.

Mechi ya Dar es Salaam Ismailia ilishinda 2-0 na mechi ya marudiano Yanga ilikomaa na kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.

 1. Yanga 3-9 Raja Casablanca-1998

Mwaka 1998 Yanga ilifanikiwa kuingia kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi B sambamba na Raja Casablanca ya Morocco. Katika mechi ya kwanza ugenini, Yanga ilichapwa 6-0, kisha sare ya 3-3 Dar es Salaam.

 1. Yanga 1-5 Zamalek-2000

Yanga ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Zamalek mwaka 2000 Kombe la Shirikisho Afrika Dar es Salaam, kabla ya kufungwa 4-0 nchini Misri.

 1. Yanga 0-3 Esperance-2007

Ilifungwa 3-0 ugenini na Esperance ya Tunisia raundi ya pili Kombe la Shirikisho, kabla ya kulazimisha sare ya bila bila Dar es Salaam.

 1. Yanga 1-2 Al-Akhdar-2008

Yanga ilikutana na Al-Akhdar kutoka nchini Libya mwaka 2008 raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).

Mechi ya kwanza ilichezwa nchini Libya na kufungwa bao 1-0, kabla ya sare ya 1-1 mechi ya marudiano.

 1. Yanga 0-4 Al Ahly-2009

Mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2009, Yanga ilipokutana tena na Al Ahly ikafungwa 3-0, kabla ya kufungwa bao 1-0 katika mechi ya marudiano.

 1. Yanga 1-3 Al Ahly-2011

Mwaka 2011,Yanga ilikutana na Al Ahly ya Misri. Katika mchezo wa kwanza ugenini Cairo, Yanga ililala 3-0, kisha ikalazimisha sare ya 1-1 nyumbani.

 1. Yanga 1-2 Zamalek-2012

Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho 2012 na kukutana na Zamalek, iliyotoka nayo sare ya 1-1 Dar, kabla ya kufungwa 1-0 ugenini.

 1. Yanga 3-4 Al Ahly-2014

Ligi ya Mabingwa 2014, Yanga ilicheza tena dhidi ya Al Ahly na kuifunga 1-0 nyumbani, kisha kupoteza kwa idadi kama hiyo ugenini. Hata hivyo iliyolewa kwa mikwaju ya penalty 4-2.

 1. Yanga 1-2 Etoile du Sahel-2015

Mwaka jana, 2015, Yanga ilikwaana na Etoile du Sahel katika hatua ya 16 bora na ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1. Ililazimisha sare ya 1-1 nyumbani na kupoteza ugenini 1-0

 1. Yanga 2-3 Al Ahly-2016

Ilikuwa ni mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Yanga ilipotoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri na kuchapwa mabao 2-1 ugenini.

 1. Yanga 0-1 Mo Bejaia-2016

Mechi hii ilichezwa usiku wa kuamkia Jumatatu Juni 20 nchini Algeria, Yanga ilipopokea kipigo cha bao 1-0 kutoka Mo Bejaia kwenye mechi ya kwanza ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ziliporudiana

jijini Dar es Salaam Yanga ililipa kisasi kwa kushinda bao 1-0, lililofungwa na  Mrundi Amis Tambwe.

 1. Yanga 1-0 MC Alger -2017

Mechi hii ilichezwa Jumamosi Aprili 8 Uwanja wa Taifa ambapo Yanga ilipata bao pekee la ushindi kupitia kwa Mzimbabwe Thaban Kamusoko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here