SHARE

NA EZEKIEL TENDWA


LICHA ya Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kuendelea kuwa kimyakimya kama vile hajui kinachoendelea kuelekea mechi yao na watani wao Simba, itakayopigwa Septemba 30, lakini siyo kweli, kwani Mkongo huyo anawakimbiza watani wao hao kimyakimya.

Timu hizo zenye upinzani wa jadi zitaumana tarehe hiyo, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sababu ya kutozungumza sana msimu huu kwa wanajangwani hao ni kutokana na kufanya usajili wa kawaida tofauti na Simba, ambao wametumia kiasi kikubwa cha fedha kuwaleta wachezaji ghali, hali inayowafanya mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi kuamini kuwa mwaka huu watatetea ubingwa wao kirahisi.

Hata hivyo, Yanga wao wanaendelea kufanya mambo yao kimyakimya bila kelele, lakini kwa umakini mkubwa, huku wakiamini kuwa Septemba 30 ndiyo wanaowabeza watajua kuwa Wanajangwani hao wapo kikazi zaidi.

Leo mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara wananoa silaha zao dhidi ya African Lyon, mchezo wa kirafiki utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Yanga kitakuwa chini ya Kocha msaidizi Noel Mwandila, kwani Kocha Mkuu Mwinyi Zahera yupo na timu yake ya Taifa ya Congo, ambayo jana ilitarajiwa kucheza dhidi ya Liberia, ambapo yeye ni kocha msaidizi wa kikosi hicho.

Licha ya kwamba yupo na timu yake ya Taifa, lakini amemuachia majukumu yote msaidizi wake na mchezo huo wa leo utatumika kama moja ya maandalizi dhidi ya kuikabili Simba Septemba 30, mwaka huu.

Zahera anatarajiwa kurejea nchini mapema wiki inayoanza kesho, akiwa na mbinu mpya ambazo atawapa vijana wake ili kuhakikisha kila timu itakayojipendekeza mbele yao haibaki salama, wakiwamo Simba.

Katika mchezo wa leo dhidi ya African Lyon, Mwandila anatarajiwa kuwachezesha vijana wake wote alionao, ukiachilia waliokwenda kuitumikia timu ya Taifa ambayo jana ilicheza dhidi ya Uganda ëThe Craneí, ugenini.

Moja ya kivutio kikubwa katika mchezo huo ni straika wao hatari, Herritier Makambo, ambaye ndiye anayeandaliwa kuwaadabisha Simba na kumzidi kete Kagere, ambaye Wekundu hao wa Msimbazi wanammwagia sifa kemkem.

Licha ya kwamba kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alinukuliwa na gazeti hili akisema haifuatilii Simba na wala hajui namna Kagere anavyocheza, taarifa za ndani kutoka kwa Wanajangwani hao zinadai kuwa hataki kuweka bayana mambo yake, kwani amekuwa akiwafuatilia kimyakimya.

Akizungumzia mchezo wa leo, mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alilithibitishia Dimba kuwa utachezwa jioni na kuwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi ili kuwaunga mkono wachezaji wao.

ìNi kweli mchezo wetu wa kesho (leo), dhidi ya African Lyon, upo palepale, ni mchezo wa kawaida wa kujipima nguvu, lakini ukiwa wa muhimu sana, hivyo tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu yao,î alisema.

Yanga wanajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui wiki ijayo ugenini, huku wakiwa wamecheza mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku Makambo akitupia bao moja na lingine likifungwa na Kelvin Yondani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here