Home Habari YANGA YAIWEKEA MTEGO MAJIMAJI

YANGA YAIWEKEA MTEGO MAJIMAJI

615
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

YANGA wanadai kuwa hali ya hewa ya mkoani Njombe, iliwafanya kuibuka na ushindi finyu dhidi ya Njombe Mji na sasa wamegundua janja janja ya kuwamaliza Majimaji ya Songea, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa Majimaji mkoani humo.

Katika mchezo wao uliopita dhidi ya Njombe Mji, Wanajangwani hao walishinda bao 1-0 lililofungwa na Ibrahim Ajib kwa njia ya faulo, huku wakilalamika kwamba baridi iliwasumbua na sasa wameamua kuendelea kukita kambi mkoani Njombe ili kuzoea hali hiyo ambayo inalingana na ile ya Songea wanakokwenda.

Yanga walicheza na Njombe Mji, Jumapili ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Sabasaba, ambapo hawajaondoka tangu siku hiyo wakiendelea kujifua mkoani humo, huku ratiba yao ikionyesha kwamba, watakwenda Songea kesho wakiwa fiti kutokana na mazoezi ya nguvu wanayopewa.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ameliambia DIMBA Jumatano kwamba kikosi chake kinachukua mazoezi jioni kwenye Uwanja huo wa Sabasaba na wanatarajia kwenda Songea kesho, huku akitamba kwamba vijana wake wapo sawasawa kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Majimaji.

“Bado hatujaondoka, tunaendelea na mazoezi yetu katika uwanja ambao tulichezea (Sabasaba), tunatarajia kuondoka Alhamis (kesho), kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Majimaji, kwa ujumla wachezaji wapo katika hali nzuri na kinachosubiriwa ni mchezo huo,” alisema.

Lwandamina amesema wachezaji wake wote aliosafiri nao wapo katika hali nzuri akiwamo Thaban Kamusoko, ambaye hakucheza mpaka mwisho katika mchezo dhidi ya Njombe Mji, kutokana na kupata majeraha wakati mpambano huo ukiendelea hiyo ikimaanisha kwamba wapo tayari kwa mapambano.

Yanga bado wana hasira kubwa kutokana na kupata matokeo ambayo wenyewe wanaona hayastahili katika michezo yao miwili iliyopita wakianza na Lipuli FC, katika mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0, dhidi ya Njombe Mji na sasa wanataka kujifariji kwa Majimaji.

Wanajangwani hao wametwaa ubingwa mara tatu mfululizo na sasa wanataka hata msimu huu wawazime wapinzani wao wa jadi Simba, ambao wamefanya usajili wa nguvu ili kukata kiu ya misimu minne mfululizo ambayo hawakunusa harufu ya ubingwa huo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here