Home Habari YANGA YAMNG’OA KIPA WA PRISONS

YANGA YAMNG’OA KIPA WA PRISONS

1267
0
SHARE

NA HUSSEIN OMAR, MBEYA

UNAWEZA kusema Yanga wana agenda ya siri na makipa wa timu ya Prisons ya Mbeya, kwani baada ya misimu miwili kutesa na aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya, safari hii wamekuja na umafia mwingine kwa Wajelajela hao.

Habari ambazo hazina mashaka ni kwamba uongozi wa Yanga juzi baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya timu hiyo na kupata ushindi mnono wa mabao 3-1, wakaanza dili la kumfukuzia kipa wao, Aron Kalambo.

Dimba Jumatano lilishuhudia baadhi ya viongozi wakifanya pilika za kuwasiliana na kipa huyo na kujiridhisha kwamba mpango mzima ni kumtaka asajiliwe katika klabu hiyo ya Jangwani ili kuongeza nguvu katika nafasi hiyo.

Hatua hiyo imefuatia kujiweka pembeni kwa aliyekuwa kipa namba moja wa Yanga, Beno Kakolanya ambaye anadai alipwe stahiki zake na klabu hiyo ndipo aendelee kuitumikia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Hussein Nyika, alilithibitishia Dimba Jumatano kuwa na mipango ya kumhitaji kipa huyo na kwamba, klabu yake itafuata taratibu zinazostahili.

Baada ya Kakolanya kujiondoa kikosini Yanga sasa imebaki na makipa wawili, Ramadhani Kabwili na Klause Kindoki ambao hapo awali hawakupewa nafasi kubwa ya kucheza.

Endapo rada za Yanga zitamnasa kipa huyo wa Prisons na kutua Jangwani, huenda akavaa viatu vya Kakolanya kwakuwa kipa namba moja, hata hivyo kulingana na falsafa za kocha Zahera, uwezo wake ndio utakaofanya apate nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here