SHARE

 

yngEMMANUEL MALIMA NA PENDO FUNDISHA, MBEYA

MABINGWA wateule wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, jana walizidi kuogesha sherehe zao za ubingwa baada ya kuibamiza Mbeya City ya hapa kwa mabao 2-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeweza kufikisha jumla ya pointi 71 ambazo haziwezi kufikishwa na timu nyingine yoyote, hivyo inachosubiri ni kukabidhiwa rasmi kombe lao.

Hadi mapumziko, tayari Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na beki Mtogo, Vincent Bossou.

Bossou alifunga bao hilo kwa kichwa dakika ya 15, akimalizia krosi ya beki mwenzake, Juma Abdul kutoka kulia aliyeanzishiwa kona fupi na winga Simon Msuva.

Hata hivyo, Yanga ililazimika kufanya mabadiliko kwa wachezaji wake wawili kipindi cha kwanza Mbuyu Tiwite na Bossou ambao waliumia na nafasi zao kuchukuliwa na Salum Telela na Kelvin Yondan.

Yanga waliuanza mchezo huo kwa kasi tangu mwanzo wakionekana kuwa na kiu ya ushindi na ndio walioanza kufika langoni mwa Mbeya City kabla ya wapinzani wao kujibu mapigo muda mfupi baadaye.

Baada ya Tambwe kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Telela, Yanga ilionekana kuongezeka ufundi hasa katikati ya dimba ambapo iliwadhibiti kabisa Mbeya City katika eneo hilo.

Baada ya mashambulizi ya hapa na pale, ndipo Bossou alipoweza kuipa timu hiyo bao la kuongoza kwa kichwa na kuifanya timu hiyo kuwa mbele.

Kuingia kwa bao hilo kuliwashtua Mbeya City ambao walijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi, lakini ukuta wa Yanga ulikaa imara na kuokoa hatari zote.

Almanusura Deusi Kaseke aiandikie Yanga bao la pili lakini akashindwa kumalizia mpira alioachiwa na Donald Ngoma, ikiwa ni baada ya Mbeya City kupoteza nafasi ya kupata goli la kusawazisha.

Hadi wakati timu zinakwenda mapumziko Yanga walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0, huku Mbeya City wakipoteza nafasi mbili za wazi na Wanajangwani hao nafasi moja.

Kipindi cha pili Yanga walirejea kwa kasi na kulishambulia lango la Mbeya City kama nyuki ambapo katika dakika ya 57, almanusura Ngoma aiandikie Yanga goli la pili baada ya kubaki uso kwa uso na kipa wa Mbeya City, Juma Kaseja, lakini akapiga mpira nje.

Baada ya kosakosa nyingi, Yanga ilifanikiwa kuandika bao la pili dakika ya 84 kupitia kwa Amis Tambwe ambaye aliachia shuti kali nje ya 18, hivyo kufikisha jumla ya mabao 21 katika Ligi Kuu msimu huu.

Mshambuliaji Mzimbabwe, Ngoma jana hakuwa mwenye bahati kutokana na kukosa mabao mawili ya wazi, moja kila kipindi wakati Simon Msuva alipoteza nafasi moja nzuri kipindi cha pili.

Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya.

Mbeya City: Juma Kaseja, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Tumba Swedi, Haruna Shamte, Kenny Ally, Suleiman Mangoma/Hamidu Mohamed dk66, Ramadhani Chombo ‘Redondo/Raphael Alpha, Salvatory Nkulula, Geoffrey Mlawa na Joseph Mahundi/Ditram Nchimbi.

2 COMMENTS

  1. Maoni:tunashukuru kwa habari mnazotupatia ila nashauri simba wampe mo timu ili waweze kushindana na azam yanga kwa sababu zinaongozwa na watu ambao wamewekeza fedha

  2. Maoni hongeren yanga kwa kutwaa ubingwa kwa mara pili mfululilizo ila nawashauri simba wampe mo timu mpira kwa sasa ni biashara

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here