Home Habari YANGA YASAJILI STRAIKA LA AFCON

YANGA YASAJILI STRAIKA LA AFCON

3895
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana walifanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola, ambaye alipewa mkataba wa miaka miwili kuihudumia timu hiyo.

Mchezaji huyo, ambaye aling’aa kwenye timu hiyo, alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliocheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa upande wa vijana wenye umri chini ya miaka 17, iliyofanyika nchini Gabon mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema kuwa, huyo ni mchezaji wa pili kuingia naye mkataba kwenye usajili huu wa dirisha dogo, baada ya Jumanne ya wiki hii kumalizana na beki wa kati kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kayembe Fiston, kwa mkataba wa miaka miwili.

Alisema sera ya Yanga kwa sasa ni kusajili wachezaji vijana zaidi ambao wanaweza kuitumikia klabu hiyo kwa miaka mingi, kuliko kukimbilia wale ambao umri umewatupa mkono.

“Sera yetu kwa sasa ni kuangalia zaidi vijana na ndicho tunachokifanya, katika usajili wa dirisha hili dogo tumepanga kusajili wachezaji watatu tu, lakini wenye uwezo mkubwa katika nafasi ya winga, beki na mshambuliaji, tunawaomba mashabiki wetu waendelee kutuamini,” alisema Nyika.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, hayo ndiyo mapendekezo ya kocha wao mkuu, George Lwandamina, kwani mpaka sasa nafasi ambayo inaonekana kusumbua sana ni ya winga, baada ya kuondoka Simon Msuva, ndiyo maana wameamua kuingia msituni kutafuta mbadala wake.

Tayari kuna majina kadhaa ambayo yametajwa kwenye nafasi hizo ambazo zinatakiwa kujazwa, akiwamo Mohamed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar, na Bitram Nchimbi wa Njombe Mji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here