Home Habari YANGA YATEKA USAJILI SPORTPESA

YANGA YATEKA USAJILI SPORTPESA

548
0
SHARE

NA MAREGESI NYAMAKA,

YANGA wanajua kuwa wanakabiliwa na michuano migumu ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kilichopo kichwani mwao ni kuhakikisha wanafika mbali na sasa wameamua kuiangalia michuano ya SportPesa kwa jicho la tatu ili kupata wachezaji wa kuwasajili.

Katika michuano hiyo inayoendelea katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Yanga, ambao pia wanashiriki, wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga AFC Leopards ya Kenya mabao 4-2 kwa njia ya penalti, baada ya dakika 90 timu hizo kutoka suluhu ya 0-0.

Yanga wanataka kuhakikisha wananyakua wachezaji wazuri kutoka timu za Kenya ambazo zinashiriki michuano hiyo, ikiwamo Gor Mahia, ambayo jana ilitangulia nusu fainali baada ya kuifunga Jang’ombe ya Zanzibar mabao 2-0.

Meneja kwa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, hawatasita kumchukua mchezaji yeyote ambaye watavutiwa naye, lengo likiwa ni kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano hiyo ya Kimataifa.

“Ni kweli michuano hii tunaifuatilia sana, ikizingatiwa kuwa hata sisi tunashiriki, na kwa sababu hiki ni kipindi cha usajili, tukiona ambaye atatufaa hatutasita kufanya naye mazungumzo,” alisema.

Yanga wanahaha kuimarisha kikosi chao, ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wachezaji wao mikataba yao imefikia ukingoni, huku baadhi yao wakionekana wazi kutaka kutimkia kwingine kutafuta changamoto nyingine.

Katika idadi hiyo ya waliomaliza mikataba yao, wapo wale ambao ndio wanaoibeba timu hiyo, akiwamo Donald Ngoma pamoja na Vincent Bossou, ambao wameshaweka wazi dhamira ya kutimka, huku Haruna Niyonzima, Thaban Kamusoko pamoja na Amis Tambwe, angalau wakionyesha mwelekeo wa kusaini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here