Home Habari YANGA YATWAA UBINGWA WA KIHISTORIA

YANGA YATWAA UBINGWA WA KIHISTORIA

261
0
SHARE

SAADA SALIM NA MAREGESI NYAMAKA,

YANGA wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa 27 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana, licha ya kupoteza mechi yake ya mwisho kwa kufungwa bao 1-0 na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Timu hiyo ya Jangwani imefanikiwa kuutetea ubingwa wake kwa mwaka wa tatu mfululizo, baada ya awali kuutwaa katika misimu ya 2014/15 na 2015/16.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na mchezaji wa Mbao FC, Habibu Haji, dakika ya 22 baada ya kuwazidi kasi mabeki ya Yanga na kupiga shuti langoni mwa Yanga lililomshinda kipa Beno Kakolanya na kuingia nyavuni.

Kwa matokeo hayo, Yanga inafanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa wastani wake mzuri wa mabao, ingawa bado kuna tishio la Simba kwenda FIFA kudai pointi tatu walizopokonywa baada ya kupewa kimakosa kufuatia kufungwa na Kagera Sugar.

Mchezo huo ulikuwa na umakini mkubwa kwa timu zote mbili, ila  ulikuja kuharibika baada ya Mbao kupata bao lao na kupelekea Simon Msuva na wachezaji wengine wa Yanga kumvaa mwamuzi wa mchezo huo, kudai penalti na kuishia kuzawadiwa kadi ya njano.

Baada ya mchezo shangwe zilitawala uwanja huo wa CCM Kirumba, huku mashabiki wa Yanga matawi kwa matawi wakiingia uwanjani kwa makundi wakishangilia na kulitembeza kombe hilo uwanjani wakiwa pamoja na wachezaji wa Mbao, ambao walikuwa wakishangilia kubaki Ligi Kuu.

Simba, ambao walimaliza wakiwa katika nafasi ya pili baada ya kuifunga Mwadui FC mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, mabao yao yalifungwa na Ramadhani Kichuya kwa mkwaju wa penalti dakika ya 12, baada ya kipa Shabani Kado kumfanyia madhambi mchezaji huyo eneo la hatari.

Dakika ya 24 Ibrahim Ajib aliifungia Simba bao la pili, akiunganisha pasi nzuri iliyopigwa na Juma Luzio. Mwadui FC nao walijipatia bao dakika ya 42 kupitia kwa mshambuliaji wao, Paul Nonga.

Kagera Sugar jana walifanikiwa kuvunja historia ya Uwanja wa Azam Complex, baada ya kuwafunga wanalambalamba, Azam bao 1-0.  Azam FC walijiwekea rekodi msimu huu baada ya kutopoteza michezo 12 mfululizo katika uwanja wao.

Matokeo hayo yameifanya Kagera Sugar kumaliza ligi katika nafasi ya tatu, wakiwa na pointi 53 na Azam FC wakichukua nafasi ya nne wakiwa na pointi 52.

Michezo mingine ni Stand United imeilaza 2-1 Ruvu Shooting Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Prisons imelazimishwa sare ya 0-0 na African Lyon Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ndanda FC imeshinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mtibwa Sugar imeshinda 3-1 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Majimaji imeshinda 2-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja Majimaji, Songea.

Kikosi kilichocheza Yanga: Beno Kakolanya, Juma Abdul, Oscar Joshua/ Emmanuel Martin, Nadir Haroub, Vicent Bossou, Thaban Kamusoka, Simon Msuva, Justine Zullu/ Deus Kaseke, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima, Anthony Mateo na Geofrey Mwashiuya.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here