Home Habari YANGA YAVURUGA KAMBI YA MBAO FC

YANGA YAVURUGA KAMBI YA MBAO FC

364
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

NI kama Yanga wameivuruga kambi ya Mbao FC kuelekea mchezo wao wa Kombe la FA, baada ya uongozi wa timu hiyo ya Mwanza kuamua kuwapokonya simu wachezaji wake kwa kuogopa hujuma.

Yanga inatarajiwa kuondoka leo kwa ndege kuelekea mkoani Mwanza tayari kuwavaa wenyeji wao hao katika mchezo utakaopigwa Jumapili hii Uwanja wa CCM Kirumba, jijini humo.

Taarifa za uhakika zilizolifikia DIMBA Jumatano kutoka ndani ya kambi hiyo, zinadai kwamba Jumatatu usiku viongozi wa Mbao walichukua simu za wachezaji wao kutokana na kuhofia kufanyiwa hujuma kuelekea mchezo wao huo.

“Wachezaji wote tumepokonywa simu na viongozi, hivyo hatutaweza kupatikana katika siku hizi mpaka mchezo huo utakapomalizika, wenyewe wanahofia kwamba huenda ikafanyika hujuma, ndiyo maana wakaamua kufikia maamuzi hayo,” alisema mmoja wa wachezaji wa Mbao, ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Alisema hiyo si mara ya kwanza kunyang’anywa simu, kwani hata mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Simba walifanyiwa hivyo hivyo, licha ya kwamba mwisho wa dakika 90 walijikuta wakiondoka uwanjani vichwa chini baada ya kufungwa mabao 3-2.

Wakati Mbao wakiwa bize kunyang’anyana simu, kwa upande wao Yanga, wanafanya mambo yao kimyakimya, wakichukua mazoezi ya nguvu kuhakikisha wanawatoa nishai wapinzani wao hao.

Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, George Lwandamina, alisema: “Tunahitaji kufanya vizuri ili kutetea ubingwa wetu, kama tukiwafunga tunakwenda fainali na hilo ndilo tunalotaka kulifanya.”

Yanga na Mbao wataingia katika mchezo huo wakiwa wameshajua nani aliyepita kati ya Simba na Azam FC, mchezo utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here