Home Habari YANGA YAWASHIKA PABAYA WAHABESHI

YANGA YAWASHIKA PABAYA WAHABESHI

6824
0
SHARE
NA CLARA ALPHONCE  |   

YANGA haitaki kurudia tena makosa katika mechi za kimataifa. Baada ya kutambua ina mtihani ujao wa mechi ya kimataifa, imeamua kufanya jambo la maana ambalo huenda likawashika pabaya wapinzani wao kabla ya kuvaana nao katika mechi ya mtoano kuingia kwenye makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga itamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mechi ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, mechi ya kwanza ikifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 7, mwaka huu na marudiano Addis Ababa kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu.

Hiyo ni baada ya droo ya mechi hizo za mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho iliyokwenda sambamba na upangwaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumatano wiki hii, mjini Cairo, Misri.

Katika kujiandaa na mechi hiyo, Wanajangwani hao wanadaiwa kufanya mambo ambayo yanaonekana kuwa ni maandalizi makini yatakayoweza kuwavusha.

Wanajangwani hao wanafahamu kwamba wakivuka hatua hiyo ya mtoano wataingia kwenye makundi na hivyo kupata kitita cha fedha ambazo zinakadiriwa kuzidi shilingi milioni 600 za Kitanzania.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa vigogo wa timu hiyo hivi    karibuni walikaa kikao na kuangalia uwezekano wa kubadilisha uwanja wa kuchezea ili kuwavuruga wapinzani wao.

DIMBA limedokezwa kuwa vigogo hao walifanya maamuzi hayo ili kuangalia uwezekano wa kusaka ushindi kwa namna yoyote ile, kwa kuwavuruga kisaikolojia wapinzani wao kulingana na hali ya hewa pamoja na uwanja, ingawa baadaye walibadili mawazo hayo na kuamua kuirejesha tena mechi jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema kazi ya kuwasoma wapinzani wao wamewaachia benchi la ufundi ambalo limeanza kazi hiyo tangu ilipofanyika droo ya michuano hiyo.

“Benchi la ufundi chini ya Kocha George Lwandamina, wapo kazini hivi sasa kuwafuatilia wapinzani na wiki ijayo baada ya timu kuanza mazoezi, tutakutana nao kwa ajili ya kutupa ripoti.

“Tumedhamiria kufanya vizuri katika michuano hiyo     kwani hatutaki kurudia makosa, tumejifunza vitu vingi mpaka hapa tulipofikia, hivyo baada ya kupata ripoti hiyo na kugawana majukumu kila mtu atapambana katika nafasi yake,” alisema Nyika.

Kwa upande wake, kocha wa Yanga, George Lwandamina ambaye yuko kwao Zambia kwa mapumziko mafupi, alisema jana kuwa atarejea haraka kesho Jumatatu ili kuiandaa upya timu hiyo kwa ajili ya michuano yote ikiwemo ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup – ASFC) pamoja na ya Shirikisho la Soka Afrika.

Lwandamina alisema atahakikisha anafanya maandalizi ya kutosha ili kuvuka hatua zote, kwani hatataka kurudia makosa yaliyowagharimu wakatolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwamba, anavyofahamu Welayta Ditcha haitakuwa ngazi ya Yanga kuwapeleka kwenye makundi.

“Kwa kufikiria ni timu kutoka Ethiopia tunaweza kuitoa ni sawa, lakini tumetazama ubora wake? Ratiba yetu yote ya msimu ilikuwa rahisi kwa kufikiria. Tuliona tumepata mpinzani rahisi kutoka Shelisheli, kadhalika na Botswana. Lakini shughuli yake tuliiona, soka imebadilika mno. Soka si maneno tena. Haihitaji dharau na mzaha. Inataka mipango, uwekezaji na maandalizi,” alisema.

Kabla ya kuwavaa Wahabeshi, Yanga Aprili 1, watacheza mechi ya Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Singida United mjini Singida na Aprili 7, watamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia.

Welayta Dicha watakuwa wanakwenda Tanzania kwa mara ya pili mwaka huu, baada ya Februari kuja kucheza na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here