Home Habari Yanga yazidi kukalia kuti kavu TPL

Yanga yazidi kukalia kuti kavu TPL

1502
0
SHARE

LULU RINGO, DAR ES SALAAM

Mabingwa wa kihistoria nchini Tanzania, Yanga Sc wamezidi kuwa na hali ngumu baada ya kupata sare ya bila kufungana katika mchezo wa leo Jumanne, Februari 6, dhidi ya Singida United mchezo uliopigwa mkoani Singida katika Uwanja wa Namfua.

Mchezo huo ulikuwa na kasi huku timu zikishambuliana kwa zamu kwa dakika zote 90 lakini bahati haikuwa kwa yeyote baada ya mpira huo kumalizika bila nyavu kutikiswa.

Sare hii ni ya pili mfululizo kwa Yanga, baada ya ile waliyoipata dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga, mpira uliomalizika wa sare ya goli 1-1, kabla ya mchezo huo Yanga alianza mzunguko wa pili kwa kupokea kichapo cha goli 1-0 kutoka kwa Stand United goli lililofungwa na nahodha wa timu hiyo Jacob Massawe.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 55 ikicheza jumla ya michezo 22, ikifuatiwa na Azam Fc iliyokwisha cheza michezo 20 na kujikusanyia alama 47 nafasi ya tatu inashikiliwa na KMC yenye alama 35 huku ikiwa imecheza michezo 23.

Takwimu hizi zinazidi kuiweka Yanga pabaya kutokana uwiano wa alama na jumla ya michezo ambayo timu zote mbili (Yanga na Azam) zimekwishacheza.

Watani wa jadi wa Yanga, Simba Sc wao wana alama 33 wakiwa na michezo nane mkononi nyuma ya Yanga anayeongoza ligi.

Kesho Alhamisi, Februari 7, Simba itashuka katika dimba la Taifa kumenyana na Mwadui FC ya mkoani Shinyanga katika mchezo wa duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here