SHARE

NA HASSAN DAUDI


 

KAMA ilivyo kawaida, kila unapomalizika mtanange wa ‘Kariakoo derby’ kati ya mahasimu wakubwa wa soka la Tanzania, Simba na Yanga, kunatokea cha kuzungumzwa kwa wiki kadhaa baadaye, ukiacha matokeo.

Safari hii, baada ya Wekundu wa Msimbazi kushinda bao 1-0 katika mchezo uliokuwa wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara, kitendo cha beki wa Yanga, Kelvin Yondani, kumtemea mate Asante Kwasi, kimebaki kuwa gumzo.

Hata hivyo, huku ikisubiriwa kuona ni adhabu gani nahodha huyo ataipokea kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), tukio hilo si geni katika mchezo wa kandanda, licha ya kwamba si la kiuungwana.

Mwaka 2003, aliyekuwa staa wa Liverpool kipindi hicho, El Hadji Diouf, alitozwa faini ya kitita cha Pauni 5,000 alipoonekana akimtemea mate shabiki wa Celtic katika mchezo wa     Uefa Super Cup.

Patrick Vieira akiwa nahodha wa Arsenal, naye aliwahi kufungiwa mechi nne na kutakiwa kulipa Pauni 30,000 alipothibitika kumfanyia hivyo staa wa West Ham, Neil Ruddock.

Hata kipa wa kimataifa wa Ufaransa ambaye ameshastaafu, Fabian Barthez, alifungiwa miezi sita kabla ya kupunguzwa na kubaki mitatu, alipogundulika    kumtemea mate mwamuzi raia wa Morocco wakati timu yake ya Marseille ikivaana na Wydad Casablanca na hiyo ilikuwa mwaka 2005.

Hata hivyo, ukiacha utovu huo wa nidhamu, yapo matukio mengine ya utovu wa nidhamu ambayo yamekuwa sehemu ya mchezo wa kandanda ulimwenguni.

Kupiga kiwiko ‘kipepsi’

Beki wa zamani wa Manchester City, Ben Thatcher, anasema  kuna wachezaji ni wataalamu wa kufanya hivyo na wao mara nyingi hutumia mipira ya vichwa. “Nikitazama mpira, naweza kumjua kabisa aliyefanya makusudi,” anasema.

Machi, mwaka jana, kosa hilo lilimgharimu Zlatan Ibrahimovic wakati alipofungiwa mechi tatu na Chama cha Soka cha England (FA), baada ya ushahidi wa video kumwonesha akimtwanga kiwiko nyota wa Bournemouth, Tyrone Mings.

Miezi nane baadaye, staa mwenzake kikosini, Ashley Young, alikutwa na hatia kwa kosa hilo pia, akafungiwa mechi tatu ilipothibitika kuwa alimfanyia uhuni huo Dusan wa Southampton.

Kumsukuma mwamuzi

Mwanzoni kabisa mwa msimu huu, Cristiano Ronaldo alizikosa mechi tano kwa kosa hilo dhidi ya mwamuzi wa ‘Classico’, Ricardo De Burgos Bengoetxea.

Ukiacha tukio maarufu la Paolo Di Canio kumsukuma mwamuzi, Paul Alcock mwaka 1998, naye kocha Arsene Wenger, alikutwa na mkasa huo wanzoni mwa mwaka jana.

Mfaransa huyo alitakiwa kuwa nje ya benchi la ufundi kwa mechi tano alipobainika kumsukuma mwamuzi wa akiba, Anthony Taylor, wakati kikosi chake kikimenyana na Burnley.

Wenger alikerwa na kitendo cha mwamuzi wa kati, Jon Moss, kumlima kadi nyekundu, lakini haikuzuia adhabu hiyo iliyoambatana na faini ya kitita cha Pauni 25,000.

Kufunga bao ‘kiujanja’

Ni utovu mwingine wa nidhamu na hapo moja kwa moja kumbukumbu za mashabiki wa soka zitawapeleka kwa mkongwe wa Argentina, Diego Maradona, kupitia bao la ‘Mkono wa Mungu’ katika mchezo wa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya England.

Baadaye, Luis Suarez naye akazuia kwa mkono mpira uliokuwa ukitinga wavuni wakati Uruguay yake ikivaana na Ghana katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010.

Ubaguzi wa rangi

Akiwa Ligi Kuu England (EPL) na Liverpool, Suarez alifungiwa mechi nane kwa ubaguzi wake wa rangi dhidi ya beki wa Manchester United, Patrice Evra.

 

Sergio Busquets aliwahi kumfanyia ubaguzi wa rangi beki wa Real Madrid, Marcelo, wakati timu zao zilipovaana katika mchezo wa Classico.

Licha ya ushahidi wa video baada ya mechi hiyo kumuonesha akimwita mwenzake ‘Momo’, yaani nyani kwa lugha ya Kihispaniola, Busquets hakuadhibibiwa na Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

Mchezaji kujifanya ameumia

Wachambuzi wa soka wanalitaja tatizo hilo kuwa ni kansa ya mchezo huo kwa sasa na linatakiwa kushughulikiwa mapema ili haki itendeke viwanjani.

Katika mchezo wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002, nyota wa timu ya Taifa ya Brazil, Rivaldo, alijitupa chini akidai ameumizwa vibaya na staa wa timu ya Taifa ya Uturuki, Hakan Unsal.

Hata hivyo, mchezo ulipomalizika na baadaye kugundulika alidanganya, alitozwa faini ya Pauni 5,180.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here