SHARE

Apotezea Kombe la Mapinduzi, asisitiza ubigwa Ligi Kuu

NA TIMA SIKILO

UKISIKIA kupandwa na hasira ndiko huku, kwani baada ya vijana wake kutupwa nje ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewaambia mashabiki wao wajiandae kufurahi kwenye michuano mingine yote iliyopo mbele yao.

Yanga wanashuka uwanjani leo kukamilisha ratiba kwenye michuano hiyo wakiwakabili Jamhuri, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.

Yanga wapo kundi B, linaloongozwa na Azam FC, wenye pointi saba, sawa na Malindi inayoshika nafasi ya pili, huku Wanajangwani hao wakiwa na pointi tatu ambapo wakishinda leo watafikisha pointi sita, ambazo hazitawasaidia kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

Kutokana na hali hiyo, Zahera amesema kwa sasa akili yake inalenga kupata matokeo mazuri katika michuano yote iliyopo mbele yao, ikiwamo ile ya Sportpesa, inayotarajiwa kuanza Januari 23 mwaka huu, Uwanja wa Taifa.

“Kwa kweli ule mchezo dhidi ya Malindi sikuuangalia (Yanga wakifungwa mabao 2-1), lakini najua tulifungwa, ila hiyo hainisumbui sana, kwa sababu mbele yetu tuna michuano ambayo naamini tutafanya vizuri zaidi.

“Tuna Ligi Kuu ambayo tumejipanga kuhakikisha tunawapa raha mashabiki wetu Michuano ya Azam (FA), lakini pia nasikia kuna Sportpesa, nadhani huku tutafanya kile ambacho mashabiki wanakitaka,” alisema.

Kuhusu kiwango cha wachezaji wake vijana wanaoshiriki michuano ya Mapinduzi, alisema licha ya kutupwa nje, lakini wameonyesha uwezo mkubwa na kama wataendelea kufanya hivyo, watafika mbali.

“Walicheza vizuri sana, isipokuwa kuna mapungufu machache, ikiwamo kukosa uzoefu, lakini naamini kama wataendelea kujituma watafika mbali, tunataka kuwalea hawa vijana ili wasiishie hapo na badala yake ikiwezekana wakacheze soka la kulipwa nje,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here