SHARE


NA MWANDISHI WETU

KOCHA Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera,siku chache baada ya kuwapiga ‘stop’ viongozi kufanya usajili wa kimataifa tayari ameshanasa vifaa vitatu kimyakimya.

Zahera ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha timu ya Taifa ya DRC kinachoijiandaa na michuano ya Afcon, alisitisha zoezi la usajili baada ya kupata taarifa kwamba, kikosi chake kitaungana na watani zao wa jadi Simba kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Kutokana na hilo ndipo akaagiza, zoezi hilo liachwe ili yeye mwenyewe ashiriki zoezi la kutafuta wachezaji wenye hadhi ya kucheza michuano hiyo mikubwa Afrika.

Habari ambazo Dimba limezipata, zinasema tayari kocha huyo ana majina matatu ya wachezaji wa nafasi tofauti kutoka nchini DRC, ambao wote ameshafanya nao mazungumzo na kufikia makubaliano.

Kocha huyo alizungumza na DIMBA Jumatano, akiwa nchini Hispania, ambako timu ya taifa DRC inajiandaa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Harambe Stars, alisema majina hayo yako tayari lakini bado ni siri yake hadi atakapoyafikisha mbele ya Kamati ya usajili.

“Sisi tuna uongozi hapo naweza mimi nikakubaliana nao kisha uongozi ukakataa nitaonekana muongo na mimi sipenzi tabia hii” alisema.

Kocha huyo pia alirudia kauli yake kwa uongozi wa Yanga akiwataka wasihofie kumtimua mchezaji yeyote atakayeonyesha nia ya kuihama Yanga kwa vile wapo wachezaji wengi wanaolilia kuchezea timu hiyo, tena wenye uwezo mkubwa.

“Mimi Zahera Mwinyi niliwaambia viongozi kuwa msiogope kwa kusikia eti wachezaji fulani wanatakiwa na timu zingine za nje kwa sababu ni za uongo, sijaona ofa yoyote, lakini pia muwaache wote wanaotaka kuondoka na mtajionea timu itakavyokuwa baada ya usajili”

Katika hatua nyingine kocha huyo alisisitiza nidhamu katika kikosi chake kipya ndiyo itakayokuwa kipaumbe ikifuatiwa na uwezo pia juhudi kwa mchezaji mmojammoja.

“Kama huku timu ya taifa DRC nasimamia nidhamu na ninaona faida yake kwa nini nikifika huko Yanga nicheke na wachezaji wazembe, niwambie tu wote watakaosaini wabadilike kabla hatujaanza program” alisema.

Zahera anatarajia kurejea nchini muda mfupo baada ya kumalizika kwa michuano ya Afcon Julai 19.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here