SHARE

NA JESSCA NANGAWE

KOCHA Mwinyi Zahera ni kama amepunguza machungu kwa mashabiki wa Yanga, hii ni baada ya kutoa kauli kuwa watarejesha heshima yao kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga kesho itakua mwenyeji wa Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru ikiwa ni mchezo wake wa pili tangu kuanza kwa ligi hiyo.

Zahera aliliambia gazeti hili kuwa, licha ya kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hawana sababu ya kuanza kusaka mchawi badala yake wanajiandaa kupambana na timu za Ligi Kuu Bara ili kulinda heshima yao.

Alisema mipango yake ni kuhakikisha wanajipanga vyema kupata ushindi katika michezo ya nyumbani na ugenini pamoja na kuelekeza nguvu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nipende tu kuwashukuru wachezaji wangu wamepambana kwa kadri walivyoweza, na imetokea bahati mbaya hatukuweza kusonga mbele, sasa kubwa ni kuangalia ligi iliyo mbele yetu pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho, kufanya kwetu vizuri kutaleta faraja kwa mashabiki,” alisema Zahera.

Aliongeza kuwa wataanza kusaka ushindi katika mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania hapo kesho huku akiahidi kurejesha furaha ya mashabiki wao kwa ushindi katika kila mchezo.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilianza vibaya ligi hiyo kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 mbele ya maafande wa Ruvu Shooting katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Saalam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here