Home Michezo kitaifa Zahera awatetea wachezaji, awaita mashabiki Taifa

Zahera awatetea wachezaji, awaita mashabiki Taifa

1607
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kushindwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Mapinduzi na ile ya SportPesa, vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, kesho wanatarajiwa kuuwasha moto watakapowakabili Biashara United, ikiwa ni hatua yao mpya ya kurejea rasmi uwanjani.

Mabingwa hao wa kihistoria ni kama vile walipotea njia, baada ya kuanza kupoteza baadhi ya mechi, ikiwamo ya ligi, hivyo mechi hii imetajwa kuwa ni maalumu kwa kuanza tena kutoa vichapo kwa kila timu itakayokuja mbele yao.

Yanga watakikabili kikosi hicho kutoka mkoani Mara, katika mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) maarufu kama FA, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo unachukuliwa na Yanga kwa uzito mkubwa, kwani bingwa wake ndiye anayeiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kutokana na umuhimu wa michuano hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alikataa katakata wachezaji wake nyota kwenda kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup, akitaka nguvu kubwa ielekezwe FA pamoja na Ligi Kuu.

Zahera ameshaweka wazi kwamba malengo yake ni kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, lakini pia Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo maana hakuonekana kuumizwa na matokeo waliyoyapata SportPesa, wakitolewa mapema na kikosi cha Kariobangi Sharks kutoka Kenya.

Katika michezo yao miwili ya mwisho, Wanajangwani hao walijikuta wakipoteza, wakianza kufungwa bao 1-0 na Stand United, Ligi Kuu na 3-2 dhidi ya Kariobangi, katika michuano ya SportPesa na sasa wanataka kurudi kwa nguvu zote katika michuano ya FA.

Zahera ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, kikosi chake kipo kamili kuwavaa Biashara United, lengo lake lipo palepale, kufanya vizuri, huku akitamba kuwa vijana wake wapo kwenye hali nzuri.

“Utakuwa mchezo mgumu, hakuna timu ya kuidharau, maana kila mmoja amejiandaa kivyake, hata hivyo kwa upande wetu tupo vizuri, tukiamini kwamba malengo yetu ya kushinda yatatimia.

“Nilishasema tangu mwanzo kwamba haya makombe mawili (FA na Ligi Kuu), tunayachukulia kwa uzito mkubwa na tutahakikisha tunafanya kile tunachohisi kitatusaidia kumaliza msimu vizuri,” alisema.

Alisema mashabiki wasiwe na wasiwasi, baada ya kikosi chao kushindwa kufanya vizuri SportPesa, kwani hiyo ilitokana na uchovu wa wachezaji wake na sasa wamejipanga kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Biashara kesho, hivyo amewaambia wamiminike uwanjani kuisapoti timu yao.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Biashara United, Amri Said, alisema kikosi chake kimekuja Dar es Salaam, kwa kazi moja tu, kuondoka na ushindi, licha ya kwamba wanakutana na timu kongwe.

“Sisi kama Biashara hatukuja kuuza sura, bali kucheza mpira, tunajua tunakutana na timu kubwa, lakini hiyo haitutishi hata kidogo, tumeshafanya maandalizi ya kutosha tukisubiri hizo dakika 90,” alisema.

Timu hizo ambazo zote zinashiriki Ligi Kuu, zina tofauti kubwa katika msimamo wa Ligi, Yanga ikiwa kileleni baada ya kucheza mechi 20 na kukusanya jumla ya pointi 53, huku Biashara ikiwa nafasi ya 18 mkiani, ikicheza michezo 23 iliyoipatia pointi 20 pekee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here