SHARE

NA ASHA KIGUNDULA

BAADA ya kutokuwa na kikosi chake kwa wiki kadhaa, hatimaye kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, anatarajia kurejea akiwa na mzuka wa hali ya juu, kuhaikisha timu yake inaanza kutoa vichapo katika kila mechi itakayocheza.

Tayari wachezaji Yanga wameshajiandaa na anayesubiriwa ni Zahera kuongoza jeshi lake na kutua nalo Mwanza kwa ajili ya mechi mbili zitakazochezwa Uwanja wa CCM Kirumba mkoani humo.

Yanga inatarajia kwenda Mwanza Jumamosi kwa ajili ya mchezo wake wa ligi utakaochezwa Jumanne dhidi ya Mbao FC, kisha wakuwa na kibarua cha mtanange mwingine wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC kutoka nchini Misri.

Ofisa Mhamasishaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz, alisema kikosi chao kitatumia usafiri wa ndege ili kutowachosha wachezaji.

Nugaz alisema maandalizi ya safari ya Mwanza yameshakamilika, anayesubiriwa ni kocha Zahera ambaye alikuwa nchini Ufaransa na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo, ambacho kilikuwa na mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ivory Coast.

Yanga wameapa kupambana kufa na kupona ili kushinda mechi zao hizo mbili lakini wakitaka waifunge mabao mengi Mbao ili kurudisha furaha kwa mashabiki na pia kujiweka vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mabingwa hao wa zamani mpaka sasa wapo katika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini wamecheza mechi tatu, wakishinda mmoja, sare mmoja na kufungwa mmoja.

&&&&&

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here