Home Makala ZIDANE AMEANZA KUMJARIBU MTU ASIYEJARIBIWA

ZIDANE AMEANZA KUMJARIBU MTU ASIYEJARIBIWA

1581
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

HUENDA Zinedine Zidane amesahau kilichowakuta watangulizi wake ndani ya Klabu ya Real Madrid, ndiyo maana ameanza kumletea utani Florentino Perez, ambaye si mtu wa kujaribiwa hata kidogo.

Ndiyo! Ameanza kuleta masihara, kwani kwa Perez kutoka sare mbili mfululizo na timu ambazo anahisi ni ndogo, tena uwanja wao wa nyumbani, ni sawa na kumjaribu rais huyo wa Klabu yenye kila aina ya utajiri.

Ni kweli kwamba ni michezo mitatu tu ambayo wamecheza mpaka sasa Ligi Kuu nchini Hispania, lakini kutoka sare michezo miwili na kushinda mmoja si jambo la kufurahisha kwa Perez.

Madrid, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini humo, walianza kwa kishindo mchezo wao wa ufunguzi baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Deportivo de La Coruna, tena ugenini na baadaye kujikuta wakipata sare mbili mfululizo.

Huenda Zidane na kikosi chake walibweteka na kujikuta sherehe yao ya kukabidhiwa kombe la ubingwa ikiingia nyongo baada ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Valencia, kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Santiago Bernabeu, mbele ya mashabiki wao lukuki.

Kama hiyo haitoshi, wakapata tena sare ya kufungana bao 1-1 na timu dhaifu ya Levante, wakiwa uwanja wao huohuo wa nyumbani, mbele ya mashabiki wao lukuki, hiyo ikiashiria kwamba mwendo wa Zidane si mzuri.

Kwa timu nyingi, hiyo si mbaya kucheza michezo mitatu na kushinda mmoja, huku miwili ikiwa sare, lakini kwa Real Madrid ya Perez, hiyo ni kama kumjaribu, kwani yeye anachotaka kukiona ni timu kushinda kila mchezo.

Alichokifanya Zidane mchezo uliopita dhidi ya Levante wa kumchezesha Marcelo kama winga, huku akianzisha baadhi ya wachezaji wa nje kama Isco, ambaye kwa sasa ni kama injini ya timu, pamoja na Karim Benzema, si dalili nzuri kwake.

Matokeo hayo waliyoyapata katika michezo mitatu yanaifanya timu hiyo kujikusanyia pointi tano, wakishika nafasi ya saba, kitu ambacho hakileti afya kwa mtu kama Perez, ambaye anaamini timu yake ndiyo bora duniani na inastahili kushinda kwa kila timu wanayokutana nayo.

Bila shaka Perez atakuwa anafuatilia nini wanachokifanya wapinzani wao ambao ni Barcelona na tayari amegundua kuwa, katika michezo mitatu waliyocheza wameshinda yote na wapo kileleni wakiwa na pointi tisa na sasa anamvutia kasi Zidane akitaka kumwambia neno.

Ni kweli kwamba Zidane ameifanyia mambo makubwa timu hiyo tangu alivyokuwa kama mchezaji ambapo tangu kizazi chake kilivyoondoka, akiwa na wakali wenzake kama Ronaldo de Lima, Luis Figo, Raul Gonzalez na wengine, Madrid haikuwa na ule msisimko wa kipindi hicho, lakini hiyo haizuii kitu kwa Perez.

Ni kweli kwamba tangu alipochukua timu hiyo akiwa kama kocha kutoka kwa Rafael Benitez, amefanya makubwa, ambapo msimu uliopita aliipa timu yake kila kitu, lakini bado hiyo haiwezi kumuweka salama mbele ya Perez, kama tajiri huyo ataona hapati furaha ya mapema.

Zidane ameipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania, La Liga, pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA), lakini anaonekana kuuanza msimu huu vibaya, huku Barcelona, ambayo ilihisiwa kwamba watachemka baada ya kuondokewa na Neymar, hali inaonekana kuwaendea vema.

Kikosi hicho leo kinaanza kutupa karata yake kutetea ubingwa wake wa michuano ya UEFA, ambapo watacheza na APOEL, kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Santiago Bernabeu, ambapo kama watapata matokeo mabaya, ni wazi Perez atainamisha kichwa chake chini, ishara ya kwamba hakubaliani na kile kinachoendelea.

Tatizo kubwa la Perez ni kwamba hataki kushindwa, hataki timu ionekane nyanya kutokana na fedha anazozimwaga kwenye usajili, ndiyo maana amekuwa mtu wa maamuzi magumu kila mara. Ole wake Zidane, kwani ni kama anamjaribu bosi wake, ambaye hajaribiwi hata kwa tone la maji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here