Home Makala Zidane Fundi aliyefanya tendo la aibu 2006 sawa na Aguero

Zidane Fundi aliyefanya tendo la aibu 2006 sawa na Aguero

481
0
SHARE
Zinedine Zidane

NA HENRY PAUL,

WAPENDA soka ulimwenguni wanapozungumzia wachezaji waliowahi kung’ara katika soka ni ngumu kuacha kutaja jina la kiungo mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Real Madrid na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Zinedine Zidane.

Ubora wa Zidane ulionekana kutokana na kile alichokuwa akikifanya akiwa ndani ya uwanja, lakini akiwa ni mchezaji mwenye kutumia akili nyingi na nguvu.

Kutokana na sifa hizo, Zidane alitunukiwa tuzo nyingi, zikiwemo Ballon d’Or 1998, Onze d’Or 1998, 2000, 2001, mchezaji bora wa Italia 1998, 2002, mchezaji bora wa michuano ya Uefa 2002, mchezaji bora wa Fifa 1998, 2000, 2003 na mchezaji bora wa Ligi Serie A 2001.

Pia mwaka 1994 na 1996, alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora kijana katika Ligi Kuu ya Ufaransa maarufu Ligue 1, mchezaji bora wa kigeni katika Ligi Kuu ya Italia Serie A mwaka 1997, 2001 na Fifa ilimtunukia tuzo ya Shaba 1997, 2002.

Tuzo nyingine ni mchezaji bora wa kigeni katika Ligi ya La Liga 2002, mchezaji bora wa michuano ya Euro 2000, 2004, mchezaji bora wa michuano ya Uefa 2001, 2002, 2003 na Shirikisho la Soka la Kimataifa linalotunza kumbukumbu, historia, takwimu za wachezaji IFFHS lilimtunukia tuzo ya mchezaji bora 2006.

Pia nyota huyo aliziwezesha timu alizochezea, hususan Real Madrid kutwaa tuzo nyingi, zikiwemo Taji la La Liga 2002/2003, Uefa 2001/2002, Supecopa de Espana 2001, 2003, Uefa Super Cup 2002 na Kombe la Mabara 2002.

Lakini pamoja na sifa zote hizo, kiungo huyo anayechukuliwa na wapenzi wengi duniani kuwa mtaalamu katika soka akiichezea Timu ya Taifa ya Ufaransa, katika michuano ya Kombe la Dunia kwenye fainali kati ya Ufaransa dhidi ya Italia alifanya jambo la aibu ambalo kamwe halitasahaulika miongoni mwa wapenda soka ulimwenguni.

Katika fainali hiyo ambayo ilichezwa dakika 120 kutokana na timu hizo kutoka  sare ya bao 1-1 dakika 90 za kawaida, nyota huyo katika dakika ya 110 alimpiga kichwa kifuani beki wa kati wa Italia, Marco Materazzi, baada ya wachezaji hao wawili kutupiana maneno huku Zidane akidai kwamba Materazzi ndiye alikuwa mchokozi.

Baada ya kitendo kile mwamuzi wa mchezo,  Horacui Elizondo, kutoka Argentina alimtoa nje kiungo huyo kwa kumwonyesha kadi nyekundu. Hivyo katika upigaji penalti tano tano Zidane hakuwepo ambapo Ufaransa ilifungwa na Italia mabao 5-3.

Kitendo kile alichofanya Zidane kilikuwa ni cha aibu mno na kiliwasononesha wapenzi wengi wa soka kote duniani, hasa  kutoka Ufaransa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa kutolewa kwa nyota huyo ndiko kulikochangia Ufaransa kukosa kutwaa taji hilo la Kombe la Dunia mwaka 2006.

Wapenzi wengi wa soka duniani kote hawakutegemea kwamba Zidane ambaye alikuwa katika kiwango kikubwa cha soka wakati huo, kufanya tukio kama lile hasa katika mechi muhimu kama hiyo.

Pia kabla ya fainali ile Zidane alikwishapewa tuzo ya mpira wa dhahabu kutokana na kucheza vizuri michuano hiyo, hivyo kitendo kile kiliwahuzunisha wapenzi wa soka Ufaransa ambapo baada ya hapo alistaafu soka.

Kitendo kile cha aibu alichokifanya Zidane katika mchezo wa fainali ile kinafanana kabisa na kitendo alichofanya mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, cha kumpiga kiwiko kwa makusudi beki wa West Ham United, Winston Reid.

Aguero alifanya kitendo hicho katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliochezwa Agosti 28 na Manchester City kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ambapo kitendo kile kilipotokea mwamuzi wa mchezo huo, Andre Marriner hakukiona, lakini mkanda wa video wa mechi ile uliporudiwa ulionyesha wazi utovu huo wa nidhamu.

Wapenzi wa soka waliohudhuria mchezo huo walihuzunishwa mno kutokana na kwamba Aguero kama alivyo Zidane naye ni mchezaji mwenye kiwango cha juu cha soka,  hawakutegemea kufanya kitendo kama kile cha utovu wa nidhamu kwa kumpiga kiwiko mchezaji mwenzake.

Hivyo kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha Aguero wa kumpiga kiwiko Reid, kumemsababishia kufungiwa mechi tatu, moja ikiwa ya wapinzani wao wakuu Manchester United utakaochezwa Jumamosi Septemba 10, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here