Home Michezo Kimataifa ZINEDINE ZIDANE ANAILAZIMISHA DUNIA IMWAMINI

ZINEDINE ZIDANE ANAILAZIMISHA DUNIA IMWAMINI

706
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA


WAKATI Manchester United ilipoboronga ilivyokuwa chini ya David Moyes, wenye timu yao waliamua kumpiga chini na kuwaachia vijana wao wa zamani wakiongozwa na Rayn Giggs kusukuma gurudumu japo kwa muda.

Giggs pamoja na wenzake Nicky Butt na Paul Scholes, waliiongoza timu hiyo katika michezo michache iliyokuwa imebakia na baada ya ligi kumalizika, aliletwa Louis Van Gaal na Giggs kuaminiwa na kuwa kocha msaidizi.

Van Gaal naye hakukawia sana dunia ikatangaziwa kuwa ametimuliwa ambapo wengi wakadhani Giggs ameshapata uzoefu na atapewa timu kuiongoza kama kocha mkuu lakini akaletwa Jose Mourinho.

Wengi walimwangalia Zinedine Zidane pale Real Madrid kwamba kama ameweza kuiongoza klabu hiyo yenye mafanikio makubwa Ulaya, iweje Giggs ashindwe kuiongoza United, lakini hata hivyo wenye timu yao wakaonyesha wasiwasi na kumnyima ulaji.

Wakati Giggs akikataa kuwa msaidizi wa Mourinho, mwenzake Zidane anaendelea kula bata pale Santiago Bernabeu, akifurahia jinsi vijana wake wakiongozwa na Cristiano Ronaldo, wakifanya kile anachowatuma.

Kama hukumbuki ni kwamba Zidane alichukua nafasi ya Rafael Benitez aliyeshindwa kuendana na kasi ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya maarufu kama UEFA Champions League na Mfaransa huyo kuanza kuiongoza kupata ushindi.

Kiungo huyo wa zamani wa Ufaransa na Real Madrid, aliyechukua nafasi ya Rafa Benitez, alikuwa amekalia benchi wakati vijana wake wakiwaangamiza Deportivo La Coruna mabao 5-0 katika mchezo wa La Liga ambao Garteh Bale alifunga matatu, huku Benzema akiongeza mawili ukawa mwanzo mzuri.

Wakati wadau wa soka wakiendelea kujisemea kimoyomoyo kwamba huenda huo ni moto wa mabua ambao muda si mrefu utazimika, wakashangaa Mfaransa huyo akinyanyua kombe la UEFA mbele ya mahasimu wao Atletico Madrid, mara hii si kama mchezaji wa Real Madrid bali kama kocha mkuu wa timu hiyo aliyoichezea kwa mafanikio makubwa.

Kilichomfukuzisha Benitez ni kutokana na timu kuwa kwenye hatari ya kushika nafasi ambayo wenyewe hawajaizoea ambapo walitolewa kabisa kwenye mbio za ubingwa wa La Liga, lakini alipoingia Zidane ghafla mambo yakabadilika, timu ikawa inashinda mfululizo na kurudishwa kwenye mbio za ubingwa na walikuja kuukosa kwa bahati mbaya.

Mafanikio aliyoyapata Zidane msimu uliopita kwa mechi chache alizoiongoza Madrid, bado watu wakadhani ni kama utani tu na msimu huu ndiyo kila kitu kitajulikana. Jambo la kufurahisha ni kwamba mpaka sasa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote La Liga wakiwa kileleni.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Madrid ilikutana na mahasimu wao Atletico Madrid na watu wa kubeti wengi wao wakaipa Atletico ushindi, wakiamini kuwa wao ni bora kuliko kikosi cha Zidane, lakini mwisho wa dakika 90 waliotabiriwa hawana lolote wakashinda 3-0, huku yule  Cristiano Ronaldo aliyekuwa akisemwa kwamba uwezo wake umepungua akifunga yote.

Licha ya kwamba tangu kupewa kikosi hicho amekuwa akifanya mambo makubwa, bado Zidane haaminiki moja kwa moja kwamba anaweza. Bado wengi wanaona kwamba hana uwezo ila ana bahati na ndiyo inayombeba.

Kama hicho anachokifanya Zidane kingekuwa kinafanywa na Jose Mourinho, Pep Guardiloa na makocha wengine wenye majina makubwa hapo kila mmoja angeamini kwamba ni uwezo wao, lakini kwa Zidane bado inaonekana anabahatisha. Hayo ndiyo madhaifu ya binadamu kutokuaminiana.

Mwanzoni mwa mwezi ujao, Madrid watacheza na Barcelona ambapo cha ajabu ni kwamba idadi kubwa ya wadau na wale wa ‘kubeti’, wataweka karata yao kwa Barcelona kushinda lakini mwisho wa dakika 90 tunaweza tena tukashuhudia miguu ikiwa juu na kichwa kuwa chini.

Wale ambao bado hawamwamini Zedane, ataendelea kuwalazimisha kumwamini kutokana na kazi yake anayoifanya na mwisho wa siku dunia itaacha kuonyesha wasiwasi na yeye na kuanza kumwamini kama wanavyoaminiwa akina Guardiola.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here