SHARE

NA ZAINAB IDDY

KARIBU msomaji wa DIMBA Jumatano na leo tumekutana tena kwenye simulizi za filamu za Kibongo.

Siku ya leo tutaiangalia filamu inayoitwa Signature iliyowashirikisha wasanii mbalimbali wakiwamo, Jacob Steven ‘JB’, Aunt Ezekiel, Jacqline Wolper, Seleman Barafu, Mussa Issa  ‘Claud 12’ na wengine.

Filamu hii inaanza kwa kuwaonyesha Aunt Ezekiel na Wolper wakiwa wanatoka uwanja wa ndege baada ya kutoka safari. Wakiwa wamefika nyumbani wanashuka katika teksi na kutakiwa kulipa fedha ambayo wanaonekana hawana hivyo wanaingia kwenye mzozo na dereva kiasi cha kushikiana visu.

Baada ya purukushani za hapa na pale, dereva anaamua kuondoka zake na Wolper pamoja na Aunt Ezekiel nao wanaingia ndani. Aunt Ezekiel na Wolper wanaonekana wakiishi maisha ya kutapeli wanaume mbalimbali kwa kutumia miili yao.

Tabia yao ni kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na wanaume na wakifika nao chumbani wanawawekea dawa za kulevya kisha kuwaibia vitu vyote vya thamani na kuondoka zao.

Siku moja Aunt Ezekiel anakutana na JB  na wanajikuta wakiwa wapenzi baada ya kuwa pamoja kwa wiki moja Aunt Ezekiel anamuwekea dawa hizo na kumwibia vitu vyote vya thamani.

Kunapopambazuka JB anagundua mwanamke aliyelala naye ameondoka bila ya kumwambia huku akiwa amemwibia vitu vyote na hivyo anaamua kuweka mitego ya kumnasa.

Siku moja akiwa katika pita pita zake anamwona Wolper na anajifanya kumhitaji kimapenzi. Bila ya kujua Wolper anakubali wawe wote na hapo ndipo JB anapoanza kuweka mitego ya kumnasa Aunt Ezekiel.

Baada ya kuzoeana naye JB anamwamrisha amwite rafiki yake ili wapange mipango ya ndoa na bila wasiwasi anafanya hivyo hivyo. Mara baada ya Aunt Ezekiel kuingia ndani mlango unafungwa ndipo Wolper na Aunt wanapogundua ulikuwa mtego wa kukamatwa.

Kwa hasira JB anampiga Aunt Ezekiel lakini pia anamtaka waweze kufanya kazi pamoja ya kuwatapeli watu mbalimbali na kujipatia pesa. Aunt Ezekiel anakubaliana na JB na kwa muda mfupi wanafanikiwa kuingiza mamilioni kwa kazi yao ya utapeli.

Siku moja JB anakwenda nyumbani kwa Aunt Ezekiel na kumwambia kuwa kuna dili la fedha wanatakiwa kulifanya lakini wanaenda kufanya na mtu wa Serikali hivyo lazima wawe makini huku akimtaka Aunt Ezekiel kuachana na rafiki zake hadi pale kazi yao itakapokamilika.

Kwa leo tunaishia hapa tukutane lakini je, ni kiongozi gani kutoka serikalini wanayepanga kumtapeli JB na Aunt Ezekiel. Tukutane Jumatano ijayo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here