SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

INAWEZEKANA kabisa mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, amekaa meza moja na Antonio Conte na kupiga stori naye huku akionyesha tabasamu, lakini ndani yake likawa na alama ya kuuliza.

Hiyo ilishatokea kwa akina Jose Mourinho, Villas Boas na wengine ambao walijikuta wakitimuliwa mchana kweupe na mmiliki huyo baada ya kushindwa kufanya kile ambacho anakitaka ndani ya kikosi chake.

Walipita makocha wengi katika kikosi hicho na kujikuta wakipoteza vibarua vyao mbele ya bosi huyo ambaye kila mara anataka timu yake itwae ubingwa kana kwamba timu nyingine hazihitaji kushinda.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Chelsea walijikuta wakifungwa mabao 3-0 na Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England, jambo ambalo liliwakera mashabiki wa kikosi hicho.

Ni wazi kwamba ushindi huo wa Arsenal haujamfurahisha kabisa Abramovich, kwani ni mtu ambaye hataki kushindwa, anatamani zile fedha zake anazozitoa kwa ajili ya usajili na mishahara zisidondoke bure, lazima zirudi na matokeo mazuri.

Sababu hiyo ndiyo ambayo iliwafanya akina Mourinho kutimuliwa, licha ya ubora wake. Kwake kutimua na kuajiri makocha wapya ni kama fasheni, bila kujua kuwa jambo hilo ni baya.

Inawezekana kabisa jicho la Abramovich limeshaanza kupepesa huku na huku kuangalia nani atamfaa kama Conte atayumba. Bosi huyu hakawii kufanya maamuzi yake ayatakayo hata kama yana athari mbele ya safari.

Conte siyo kocha mbaya, ni moja ya makocha wazuri, lakini bahati mbaya kwake ni kwamba amekwenda kwenye timu ambayo anayeimiliki anataka matokeo ya haraka. Hili ndilo tatizo ambalo linaweza kujitokeza.

Ni kweli kwamba Ligi bado ni mbichi, kwani kila timu imecheza michezo mitano lakini Abramovich huwa anataka kuona timu yake ikiwa inaongoza ligi au nafasi ya pili na ya tatu, vinginevyo haelewi kabisa.

Katika michezo hiyo sita ambayo wamekwisha kucheza, wana pointi 10 kwenye nafasi ya nane, huku Manchester City wakisimama kileleni na pointi zao 18, jambo ambalo Conte anaweza akakumbana na swali kwamba kwanini isiwe Chelsea kileleni na badala yake iwe Man City?

Mwishoni mwa wiki hii Chelsea wanakabiliwa na kibarua kingine dhidi ya Hull City ugenini, ambapo kama watapoteza tena, ni wazi Conte atazidi kuwa kwenye wakati mgumu na haitashangaza akianza kupigiwa mahesabu ya kufukuzwa.

Kichwa cha Abramovich anakijua mwenyewe. Huwa hana muda wa kupoteza, unaweza ukacheka naye leo, kesho akakubadilikia na kukuambia ufungashe kila kilicho chako upakie ndege utimke zako.

Hakuna aliyetegemea kwamba Mourinho angeondoka kwa jinsi walivyokuwa wakipendana, lakini kama Waswahili wanavyosema ‘hayawi hayawi mwisho huwa’, ndicho kilichotokea.

Ni kweli Conte amesema anahitaji muda wa kukisuka kikosi hicho, kwani ndiyo kwanza amekabidhiwa jukumu hilo, lakini amekwenda kwa mtu ambaye huwa hana tabia za kutoa muda mrefu. Yeye anachojua ni kumwaga fedha na kuletewa ubingwa tu.

Abramovich hataki kuona timu kama Manchester United, Man City, Arsenal na timu ndogo zikiwa juu yake, hivyo kuna hatari kubwa kwa Conte kukumbana na panga kali lililowakata akina Mourinho kama hataamka angali asubuhi.

Abramovich anajua kwamba msimu uliopita timu yake ilifanya vibaya na kumaliza nafasi ambayo hataki kusikia kabisa ikijitokeza msimu huu, hivyo kama kuna kusuasua kwa namna yoyote huwa kunamuumiza kichwa.

Ni kweli kwamba Chelsea wamecheza michezo sita kama ilivyo kwa timu nyingine, lakini anatakiwa kujiangalia mara mbilimbili yasije yakamkuta yaliyowakuta watangulizi wake.

Utakuwa hujakosea kama ukisema Abramovich anakwenda na kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’. Ukifanya vibaya unatumbuliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here