SHARE

NA WINFRIDA MTOI

HESABU za Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, si za nchi hii aisee, akithibitisha hilo alipofichua siri ya kwenda kucheza mechi za kirafiki mkoani Kigoma.

Wakati wapenzi wengi wa soka, wakiamini safari hiyo ilikuwa ni maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC, lakini kuna kilichojificha nyuma ya pazia.

Wakiwa mkoani Kigoma, Simba walicheza mechi mbili za kirafiki kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, ilianza na Mashujaa FC, ikaibuka na ushindi wa bao 1-0, baada ya hapo wakakutana na Eagle Noir ya Burundi, ikamalizika kwa suluhu.

Wekundu wa Msimbazi hao wanatarajia kukutana na Azam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tayari Aussems ameweka bayana kuwa amekamilisha maandalizi ya mchezo huo, akifurahishwa zaidi, kurejea kwa nyota wake waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa.

Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika asubuhi, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kocha huyo alionekana akiwa pembeni akifuatilia kile kinachofanyika, akimpa nafasi kubwa msaidizi wake, Denis Kitambi kutoa maelekezo wakati wa kucheza mechi.

Kutokana na vikosi viwili alivyopanga Aussems jana, ilionyesha wazi jeshi lake litakaloivaa Azam ni lipi, kulingana na aina ya wachezaji.

Katika mazoezi hayo ambayo BINGWA ilishuhudia, kikosi cha kwanza kiliundwa na Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Gerson Fraga, Deo Kanda/Miraji Athuman, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Mzamiru Yassin na Ibrahim Ajib.

Kuelekea mechi hiyo, wachezaji kama Shomari Kambombe anaweza kukosekana kutokana na jana kushindwa kufanya mazoezi na wenzake, kichwa kilikuwa kinamuuma na alibaki ndani ya gari.

Wengine ni Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco ambao ni majeruhi, huku Clatous Chama akionekana bado hajawa fiti kutokana na kukosekana mazoezini muda mrefu.

Akizungumzia mchezo huo, Aussems, alisema utakuwa mgumu, timu anayokutana nayo ni nzuri, pia kuna nyota atawakosa, lakini yeye ni kocha anajua aingie na mbinu gani ili kupata ushindi.

Alisema mipango yake ni kuendeleza pale walioishia katika matokeo waliyopata mechi nne zilizopita, lengo ni kwenda mbele na si kurudi nyuma, hivyo siku zote za maandalizi ni mikakati ya mchezo huo na mingine.

“Hakuna asiyeijua, Azam ni timu nzuri, ina wachezaji wazoefu, hivyo natarajia mchezo mgumu ila tumejiandaa kukabiliana nao, wachezaji wangu wako fiti japo nitawakosa baadhi ni majeruhi kama Mkude na Tshabalala,” alisema Aussems.

Katika hatua nyingine, Mbelgiji huyo, alisema safari yao ya Kigoma itakuwa na faida kubwa kutokana na alivyoona aina ya viwanja vya mikoani.

Alisema viwanja vingi vinawapa wakati mgumu wachezaji na kushindwa kucheza kwa ufanisi kwa sababu ni vibaya, lakini wameutumia Uwanja wa Lake Tanganyika kama sehemu ya mazoezi katika mechi mbili walizocheza.

“Baadhi ya viwanja vya mikoani si vizuri, vinatupa wakati mgumu, ila nimejipanga, umeona hata uwanja tuliotumia Kigoma ni mbaya, wachezaji wangu walipata shida lakini wamecheza vizuri.

“Imekuwa moja ya mazoezi kwao kuelekea mechi ambazo tutacheza nje ya Dar es Salaam, tutakutana na viwanja vya tofauti,” alisema.

Baada ya mchezo na Azam, Wekundu wa Msimbazi hao, wanatarajia kukutana na Singida United kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Shinyanga ambao ni kati ya viwanja vinavyolalamikiwa kuwa ni vibovu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here