SHARE
NA SAADA SALIM

HALI ya Rais wa Simba, Evance Aveva, ambaye yupo mahabusu si nzuri, baada ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa Temeke, kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.

Mmoja wa watu wa karibu wa Rais huyo, Alhaj Hassan Mnyenye, ameliambia DIMBA kwamba ndugu yake huyo alipelekwa hospitali hapo juzi na jana baada ya hali yake kuwa mbaya.

“Ni kweli hali ya Aveva si nzuri, hivyo baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya magereza walimpeleka Hospitali ya Temeke kwa ajili ya vipimo na matibabu na kwa sasa amelazwa wodi namba tatu,” alisema Mnyenye.

DIMBA lilimtafuta Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk. Juma Alli Malewa, ambapo alisema yeye hana taarifa hizo lakini hilo ni jambo la kawaida kwa mahabusu yeyote kupelekwa hospitalini kama akiumwa.

“Mgonjwa kupelekwa hospitalini si lazima Kamishna ajue, ni jambo la kawaida kwani anaenda huko kutibiwa kama mahabusu wengine wanavyotibiwa wakiwa wanaumwa,” alisema Malewa.

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Hajji Manara, alisema hafahamu lolote kwani yupo Zanzibar na timu ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

“Kusema kweli sifahamu taarifa hizo kwani nipo Zanzibar na timu, subiri niulize wenzangu waliopo Dar es Salaam, kama wana taarifa hizo nitakutaarifu,” alisema Manara.

Aveva ambaye bado yupo mahabusu katika Gereza la Keko Wilaya ya Temeke na makamu wake, Geofrey Kaburu, walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya utakatishaji fedha kiasi cha dola 300,000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here