SHARE
kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor ‘Cheche

NA JESCA NANGAWE

BAADA ya kutupwa nje kwenye michuano ya Mapinduzi ambayo inafikia tamati kesho, waliokuwa mabingwa watetezi, Azam FC, wameamua kuelekeza akili zao Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wanalambalamba hao walijikuta wakikwaa kisiki kwa Simba wakikubali kichapo cha mabao 3-2 kwa mikwaju ya penati hatua ya nusu fainali baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa 0-0.

Akizungumza baada ya kupokea kichapo hicho kutoka kwa Simba, kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor ‘Cheche’, alisema kwasasa akili zao wanazielekeza Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya FA.

“Kwanza tunashukuru kwamba vijana wamepambana kwenye michuano hii ya Mapinduzi lakini bahati haikuwa upande wetu lakini sasa akili zetu tunazielekeza Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na FA,” alisema.

Waliofunga penalti za Azam FC katika mchezo huo dhidi ya Simba ni mabeki Mghana Yakubu Mohamed na Mzimbabwe Bruce Kangwa, wakati Iddi Kipagwile aligongesha mwamba wa chini, mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma akapaisha juu ya lango kabla mkwaju wa kipa Razack Abalora kuokolewa na Beno Kakolanya.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Azam FC, wamecheza michezo 13 wakishinda michezo nane, sare michezo miwili huku wakipoteza michezo mitatu, wamejikusanyia jumla ya pointi 26 wakipitwa kwa jumla ya pointi tisa na Simba waliopo kilele na pointi zao 35 wakicheza michezo 13.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here