SHARE

NA SAADA SALIM

BARUANI Akilimali ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na Yanga akitokea katika kikosi cha Kigoma Kombaini, kwa lengo la kuziba nafasi ya winga Simon Msuva aliyepata nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Difaa El Jadid, nchini Morocco.

Akilimali ni mdogo wa mchezaji wa zamani wa Simba, Yahaya Akilimali, ambaye aliichezea Wekundu wa Msimbazi kwa mafanikio.

Mchezaji huyu ambaye ni mfupi kwa kimo, amekuwa kivutio kwa namna anavyojituma mazoezini kiasi cha kuwafanya mashabiki kuamini ni mtu sahihi anayeweza kurithi nafasi ya Msuva.

Breaking News ya DIMBA Jumatano ilifanya mahojiano na winga huyo aliyekuwa nchini Uganda katika masomo na kuzungumza mambo mbalimbali ikiwamo maisha yake ndani na nje ya soka.

Kuhusu kupewa uraia wa Uganda:

Akilimali anasema baada ya kufanya vizuri katika mchezo wa mpira wa miguu akiwa Shule ya Sekondari ya St. Michael, nchini Uganda, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), lilitaka kumpa uraia ili aweze kuchezea timu yao ya taifa ya vijana.

“Unajua wenzetu Waganda wanafuatilia sana michezo shuleni hususan soka, ambapo wanaenda katika mashindano hayo na kuangalia vipaji kwa ajili ya kuunda kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20,” anasema.

Akilimali anasema baada ya kuonekana katika mashindano ambayo alionyesha kiwango kizuri, Fufa walimfuata na kutaka kumfahamu vizuri na walipogundua ni Mtanzania, walihitaji abadili uraia ili wamjumuishe katika orodha ya kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20.

“Niliwasikiliza vizuri mazungumzo yao lakini sikuwajibu kwa wakati, kwa sababu kila kitu changu kuhusu suala la soka nilikuwa nikishauriana na mwalimu wangu wa michezo, pia sikutaka kujifunga kutokana na ndoto zangu kwamba siku moja nije kuchezea taifa langu.

“Mara nyingi huwa najivunia Utanzania wangu hata tukiwa katika mashindano ya kawaida darasani hali ilikuwa hivyo hivyo, nilikuwa nawakilisha na kutangaza nchi yangu na ndiyo sababu kubwa ya kukataa kubadili uraia nikiamini ipo siku soka litanitoa,” anasema Akilimali.

Kwanini Yanga na si Simba:

Winga huyo anasema amesaini Yanga mara baada ya kufuatwa na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo kuhitaji kufanya naye akisisitiza wanahitaji huduma yake.

“Kabla ya kutua Yanga ambapo nimesaini mkataba wa miaka miwili, nilifanya majaribio na Mtibwa Sugar ambapo niliambiwa niache mawasiliano yangu lakini hadi sasa sijapata majibu yoyote,” anasema.

Misumari (ushirikina):          

Winga huyo anasema suala hilo kwake halimpi shida kutokana na kutoamini imani hiyo licha ya nchi za Afrika hivyo vitu vipo.

“Huyo anayekwenda kupiga misumari ni mwanadamu anayemuomba Mungu, hivyo kila jambo kwangu namwanchia Mungu na anajibu kwa muda wake. Kikubwa nitahakikisha nafuata maelekezo ya kocha na kusaidia timu yangu kufanya vizuri,” anasema Akilimali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here