SHARE

NA JESSCANANGAWE

NAHODHA na straika wa Simba, John Bocco, amewapigia magoti mashabiki na viongozi kutokana na timu yao kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Bara.

Bocco ambaye katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting alikosa penalti, alikiri ni wazi hata wao wameumizwa na aina ya matokeo waliyoyapata.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Bocco alieleza masikitiko yake ya kupoteza alama sita katika michezo miwili na kuahidi kupambana kuirejesha timu kwenye morali ya ushindi.

“Kwanza nimshukuru Mungu kwa kuwapa moyo wa upendo Wanasimba wote wa kuipenda timu yetu na kuiunga mkono, kwa niaba ya wachezaji niseme tunaomba mtusamehe kwa matokeo tuliyopata ya michezo yote miwili iliyopita,” alisema Bocco.

Bocco aliongeza, “Tuliteleza na tumeshateleza hatupaswi kuteleza tena na hii ndio ahadi yetu kwenu kurekebisha makosa yetu na kurudi wenye sura mpya na upambanaji mpya kwa michezo yote ijayo ili turudishe furaha yetu kwa kupata matokeo mazuri kama tulivozoea.”

Aidha Bocco alikiri kuwa anatambua kupoteza michezo miwili ni pengo kubwa lakini watapambana kurejesha morali ya timu katika michezo yote iliyosalia.

Simba ipo nafasi ya nne ikiwa na alama 13 huku Azam FC wakiendelea kukaa kileleni na alama zao 21 wakati Yanga inashikilia nafasi ya pili kwa alama 19 na Biashara United ni ya tatu kwa alama 16.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here