SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KUTOKANA na tetesi mbalimbali kuhusu usajili wa kikosi cha Simba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mbatha, amefunguka kuwa wanachosubiri ni ripoti ya mwalimu ili kuanza mambo haraka iwezekanavyo.

Kumekuwa na tetesi za wachezaji tofauti wakihusishwa kutua katika kikosi hicho cha mabingwa mara tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lengo likiwa ni kujiimarisha kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa mazoezi ya mwisho msimu huu  kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea mikoani, Senzo alisema suala la usajili halikwepeki kutokana na timu watakazochuana nazo.

Alisema katika usajili wao, kikosi cha msimu ujao kinatarajia kuwa na wachezaji wasiozidi 30 na wote wawe na viwango vya juu vya kushindana kimataifa.

Senzo alieleza kuwa baada ya kumaliza mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi Namungo FC mjini Sumbawanga, Kamati ya Usajili itakaa na kupitia ripoti ya mwalimu na kuanza mipango ya usajili haraka kwa wachezaji wanaowataka.

“Mimi nahusika zaidi na mambo ya uongozi, kuhusu wachezaji wa nafasi zipi wanasajiliwa ni hadi tutakapopitia ripoti ya mwalimu kama kamati, ninachoweza kusema ni kwamba kikosi chetu msimu ujao hakitazidi wachezaji 30.

“Ninachotakiwa ni kutengeneza mazingira mazuri ya kocha kufanya kazi yake vizuri, lakini baada ya mambo yote kukamilika kila kitu kitawekwa hadharani, kama ni wachezaji wa nje au ndani,” alisema Senzo.

Wakati huo huo, Senzo alisema kuna faida ya kumiliki viwanja vya mazoezi kwa klabu za Ligi Kuu Bara na kuzishauri ambazo hazijafanya hivyo zijitahidi kuhakikisha zinamiliki.

Alisema unapofanya mazoezi katika uwanja wako, unakuwa huru na kutengeneza timu kadri unavyotaka tofauti na kutumia viwanja vya kukodi.

“Ni muhimu sana kuwa na uwanja wako wa mazoezi, unapanga ratiba zako unavyotaka, unaanda timu unavyotaka bila usumbufu, nazishauri klabu nyingine hususan za Ligi Kuu Bara kujaribu kuwa na rasilimali zake kama uwanja.

“Hii inasaidia pia kuepuka gharama zisizokuwa za lazima kwa sababu utatumia fedha tena kulipia eneo la kufanyia mazoezi ambazo utaweza kuzifanyia mambo mengine,” alisema Senzo.

Alifafanua kuwa mafanikio waliyopata msimu huu ikiwamo kutwaa ubingwa, yamechangiwa pia na kufanya mazoezi katika uwanja wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here