SHARE

MANCHESTER, England

KIPIGO cha mabao 2-0 walichokipata Manchester United dhidi ya Burnley katika Uwanja wa Old Trafford, Januari mwaka huu kiliongeza presha kwa Ole Gunnar Solskjaer ambaye alitabiriwa kufukuzwa ndani ya kikosi hicho cha mabingwa mara 20 wa Ligi Kuu England.

Mbaya zaidi, mpaka mechi hiyo inamalizika, siti za mashabiki ndani ya Old Trafford zilibaki nusu bila watu, lakini haikutosha, kwani hata mashabiki waliobaki walipaza sauti zao, wakiwazomea wachezaji wao walipokuwa wakielekea vyumbani.

Mashabiki walionesha chuki, walishindwa kuzuia hisia zao, walivurugwa haswa. Pengine ni kati ya michezo ambayo kikosi cha Manchester United kilicheza vibaya msimu huu. Lakini, hali inaonekana kubadilika sasa.

Katika kipindi ambacho kabla michezo haijasimamishwa, Manchester United walikuwa kwenye ubora mkubwa huku wakiwa na uhakika wa kuingia ‘top four’, walifika robo fainali ya Kombe la FA na walikata tiketi ya kufika nane bora ya michuano ya Ligi ya Europa.

Solskjaer hakuwa mnyonge tena, kwani, aliiongoza timu hiyo michezo 11 bila kupoteza. Ni mechi nyingi tangu kocha huyo raia wa Norway apewe mkataba wa kudumu ndani ya Old Trafford.

Hayo yote yasingewezekana bila uwepo wa Bruno Fernandes. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 alibadili upepo wa hofu, chuki na moyo kuvunjika tangu alipokanyaga nyasi za Uwanja wa Old Trafford kwa kitita cha pauni milioni 68 akitokea Sporting Lisbon ya Ureno.

Katika michezo tisa ya michuano yote aliyovaa jezi ya Manchester United, amefanikiwa kufunga mabao matatu na kutoa asisti tano na kufanya mambo mengi ndani ya timu hiyo.

KAONGEZA KILICHOKOSEKANA

“Tunahisi kaongeza kilichokosekana na ubora zaidi,” alisema Solskjaer, Februari mwaka huu. “Anatupa ladha tofauti. Ni mchezaji anayependa kucheza pasi za kupenyeza na kuelekea mbele, anapenda zaidi kujitoa, jambo ambalo linatakiwa kufanywa na mchezaji wa Manchester United.”

Bruno anafanya mambo ambayo yanatakiwa kufanywa na wachezaji wanaovaa jezi ya Manchester United, tofauti na ilivyokuwa hivi karibuni kabla ya ujio wake.

Ubunifu ulikosekana katika eneo la kiungo, bila Paul Pogba, lakini Fernandes amebadili kila kitu tangu aingie kwenye timu. Mchezo wake wa kwanza, inawezekana ulisahau kama ulimalizika kwa suluhu dhidi ya Wolverhampton.

Bruno aliweza kumtafuta Juan Mata kwa pasi za kupenyeza katika ya mstari, aina ya pasi ambazo ni ngumu kuonekana na mchezaji mwingine.

Kweli, kilikuwa kitu kilichokosekana. Jambo kubwa zaidi anafunga na kutoa pasi za mabao ‘asisti’. Ndani ya Ligi Kuu England, Fernandes anaongoza katika orodha ya wachezaji wa Manchester United kwa kupiga mashuti, kutengeneza nafasi na pasi ndani ya eneo la tatu la wapinzani.

Ni jambo ambalo limekuwa na mwendelezo mzuri tangu alipofika, amepiga pasi ndani ya boksi, mara tatu zaidi ya wachezaji wenzake. Katika Ligi Kuu England, amefanya hivyo mara 48, akiwa nafasi ya pili nyuma ya beki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold. Hizo takwimu tangu mwanzo wa Februari.

Fernandes ameiunganisha timu kutoka katika kiungo mpaka kwenye ushambuliaji, lakini uwezo wake wa kuzalisha pasi za mwisho unamuweka kundi tofauti na wengine.

Alipokea pasi katika eneo gumu la ulinzi, lakini alifanikiwa kumtafuta Anthony Martial ambaye alifunga bao la tatu dhidi ya Watford na aliweza kupiga kona ambayo ilifungwa na Harry Maguire dhidi ya Chelsea katika ushindi wa mabao 2-0.

Ghafla, Manchester United wamebadilika, wamekuwa timu inayoshambulia kwa mara nyingine. Ndani ya michezo nane ambayo Fernandes alianza, walifunga mabao 21.

United walikuwa na wastani wa 1.6 wa kufunga mabao, lakini sasa wamesogea hadi 2.6. Odion Ighalo amechangia kwa kiasi kikubwa pia, ndio, lakini mabadiliko yote yameletwa na mchezaji mmoja.

AMEONGEZA NJAA NA UONGOZI

Ubora wa Fernandes hauna maswali, hilo linajulikana. Huyu ni mchezaji aliyefunga mabao 63 na kutoa asisti 52 katika michezo 137 aliyocheza akiwa na jezi ya Sporting Lisbon.

Lakini ndani ya historia ya United ilithibitishwa uwezo si jambo pekee linalotosha. Jambo la kushukuru kipaji cha Fernandes kimefanikiwa walipofeli akina Alexis Sanchez, Angel Di Maria na wengine.

“Tulikuwa tukizungumza kuhusu wachezaji wanaohitaji muda kuzoea ndani ya timu, vipi haijamchukua muda mrefu Bruno? Alisema Roy Keane katika mahojiano na Sky Sports, mwezi uliopita. “Anaonekana ni mtu wa kipekee, ni uhamisho mkubwa kwake, lakini anaonekana kufurahia, anaonesha kuwa na njaa na tamaa ndani yake.”

Hilo lilithibitika pale alipokwaruzana na kutupiana maneno na kocha wa Manchester City, Pep Guardiola katika mchezo wa Manchester Derby ambao United walishinda mabao 2-0.

“Namuheshimu Pep, kwa makombe aliyoshinda na mambo aliyoyafanya katika mchezo huu, lakini alishindwa kuniheshimu na mimi nahisi hakuhitaji heshima yangu,” aliongea Bruno alipohojiwa na Sky Sports.

Mabadiliko hayo yamerudisha furaha kwa mashabiki ambao tayari huimba jina lake, pia, hata wachezaji wenzake wamekuwa na maoni mauzri juu ya uwepo wake katika kikosi hicho cha Mashetani Wekundu.

“Ana ubora mkubwa ndani yake,” alisema nahodha wa Manchester United, Harry Maguire. Luke Shaw naye hakuwa nyuma kummwagia sifa “Ni mtu muhimu katika vyumba vya kubadilishia nguo, hata ndani ya uwanjani.” Upande mwingine, kipa David de Gea aliongeza “Bruno ni mchezaji tofauti.”

Fernandes amekuwa akipokea sifa kutokana na utendaji wake wa kazi katika mechi mpaka uwanja wa mazoezi, ana nguvu na hushiriki pia katika kuzuia kama anavyofanya kwenye kushambulia.

Mpira ukiwa miguu mwake ni sehemu salama, ubora mkubwa wa kuwaongoza wengine ni kitu kilichokosekana. Amekuwa bora katika kila kitu, wote waliomzunguka wananufaika na uwepo wake.

“Ameongeza uongozi, lakini ameupeleka kwa njia tofauti, watau wanadhani kuwa kiongozi lazima upambane kwa kukaba, lakini amekuwa chachu ya kiwango bora kwa wengine, hayo yametokana na ubora alionao ndani ya kikosi hicho,” alisema Keane.

Hivi karibuni, Martial alionekana asiyefaa, lakini katika michezo sita ya mwisho kabla ya msimu kusimama, straika huyo raia wa Ufaransa amefunga mabao manne, huku matatu yakitokana na Fernandes.

Katika eneo la kiungo, Fred amekuwa bora na Nemanja Matic amesimama imara zaidi. Upande wa kulia, kwa kiasi Fulani, Aaron Wan-Bissaka ameimarika katika eneo la ushambuliaji na akifanikiwa kutoa asisti mbili. Yote hayo ni uwepo wa nyota huyo mpya raia wa Ureno.

Hata hivyo, yote yanafanyika kwa ajili ya timu. Manchester United ndiyo wanaopata faida zaidi. Yale makelele ya mashabiki na kuzomewa wachezaji ndani ya Old Trafford dhidi ya Burnley yamekuwa kumbukumbu sasa.

Mchezo wa soka ukirejea tena na Bruno Fernandes akiwaongoza wenzake, Manchester United wanaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kumaliza juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku wakiwa na matumaini ya kushinda mataji wanayoshiriki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here