SHARE

MADRID, Hispania

KLABU ya Real Madrid imekamilisha dili la kumsajili mpachika mabao hatari kutoka Eintracht Frankfurt, Luka Jovic, uhamisho uliowagharimu mabingwa hao wa kihistoria wa Ulaya kitita cha pauni milioni 62.

Straika huyo atajiunga na vigogo hao wa Hispania kwa mkataba wa miaka sita akitarajia kufanyiwa vipimo siku chache zijazo, baada ya klabu zote kumalizana jana asubuhi.

Dau la pauni milioni 62 za uhamisho ni kubwa zaidi ya yote ambayo Madrid iliwahi kulipa kwa ajili ya kusajili straika. Na pia atakua mchezaji wao wa tatu wa thamani kubwa nyuma ya Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.

Mserbia huyo anaiacha Eintracht Frankfurt katika kibarua kingine cha kusaka mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha kutikisa nyavu, ambapo mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Fredi Bobic alisema: “Tumehuzunika kuondokewa na Jovic.”

“Kasi yake na ufundi wa kupachika mabao vilishangaza Ulaya nzima. Hata hivyo, si mabao yake tu yaliyotufaidisha katika kipindi cha miaka miwili aliyokuwepo hapa.

“Ametuachia fedha nyingi sana za uhamisho wake. Tunamtakia kila la kheri. Ni mchezaji mwenye kila sifa ya kuchezea timu kubwa na tunajivunia kuwa naye pamoja hadi atakapostaafu,” alisema Bobic.

Jovic alijizolea umaarufu mkubwa Barani Ulaya na hasa kwenye soko la washambuliaji baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu akiwa na Frankfurt msimu huu.

Katika mechi 32 alizoitumikia klabu hiyo kwenye Bundesliga, Jovic aliweza kufunga mabao 17 na mengine 10 katika mitanange 14 ya Ligi ya Europa na kuisaidia Frankfurt kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

Alianza kucheza soka katika timu ya Red Star Belgrade ya Serbia, kabla ya kujiunga na wababe wa Ureno, Benfica na kusogea hadi Frankfurt kwa mkopo kabla ya kusajiliwa jumla mwaka huu.

Akiwa ndio kwanza na umri wa miaka 21, Jovic tayari ana medali za ubingwa wa SuperLiga (Serbia), Primeira Liga (Ureno) na DFB Pokal ya Ujerumani, huku akiwa ameitwa mara kadhaa kwenye timu yake ya taifa ya Serbia.

Ni wazi straika huyo atakua tayari kwa kazi iliyompeleka Madrid hasa katika kipindi hiki ambacho kocha, Zinedine Zidane anatengeneza timu imara itakayofanya vizuri zaidi msimu ujao.

Zidane alirejea Madrid na kuikuta timu hiyo ikiwa kwenye hali mbaya ambapo iliweza kumaliza msimu uliopita wa La Liga katika nafasi ya tatu.

Baada ya usajili huo wa Jovic ambaye ameungana na beki, Eder Militao aliyetokea Porto, sasa Zidane anatazamia kukamilisha dili lingine kubwa la staa wa Chelsea, Eden Hazard.

Hazard bado ni mchezaji anayefuatiliwa kwa ukaribu na miamba hao wa Hispania ambao wanatarajiwa kumnasa Mbelgiji huyo kwa kitita cha pauni milioni 100.

Hata hivyo, ili aweze kumpata mchezaji mwingine, Zidane atahitajika kuwauza baadhi ya mastaa wakiwemo Bale na Keylor Navas.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here