SHARE
Frank Lampard

LONDON, England

WENGI hawakujua kipi Frank Lampard ataingia kukifanya ndani ya kikosi cha Chelsea alipokabidhiwa timu hiyo baada ya Maurizio Sarri kuondoka kujiunga na wababe wa Itali, Juventus msimu huu.

Kwa jinsi mambo yanavyoenda ndani ya kikosi hicho, Chelsea wapo nafasi ya nne, pointi tatu mbele ya Manchester United waliopo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Wakati huu ambao timu inategemea kufuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, Lampard anaonekana kuamini wachezaji vijana na kuna uwezekano baadhi ya nyota tusiwaone Stamford Bridge msimu ujao.

Makala haya yanakuletea wachezaji wanne ambao wanatakiwa kufunguliwa milango ya kuondoka Stamford Bridge na Lampard ili ajenge kikosi chake.

PEDRO

Pedro Rodriguez alikuwa mmoja wa wachezaji vipenzi vya mashabiki tangu aliposajiliwa mwaka 2015. Alitokea Barcelona, aliwasili akiwa na kiwango cha juu sana ndani ya Chelsea na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kikosini.

Kwa kipindi alichokuwa Chelsea, ameshinda mataji ya Ligi Kuu England, Kombe la FA na Europa League. Mpaka sasa ametimiza miaka mitano akiwa na jezi ya klabu hiyo yenye maskani yake London.

Hata hivyo katika umri wake wa miaka 32, hakuna kingine cha ziada ambacho winga huyo anaweza kutoa kuwa na msaada ndani ya Chelsea.

Msimu huu, amefunga bao moja tu katika michezo tisa ya Ligi Kuu England aliyocheza, ndio maana Lampard amekuwa akiwapanga mara kwa mara Tammy Abraham na Mason Mount kubeba mzigo wa timu hiyo.

MARCOS ALONSO

Ingawa amekuwa katika kiwango kizuri kipindi cha karibuni, lakini si mchezaji ambaye anaweza kuitoa Chelsea sehemu moja kuipeleka kwingine kwa maendeleo zaidi.

Lampard anaijenga timu imara zaidi, ndio maana mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ameishia kuwa sehemu ya nyota wa akiba kwa muda mrefu akimpisha kikosini Emerson.

Chini ya Antonio Conte, beki huyo raia wa Hispania alikuwa akitumika zaidi kama wing-back wa kushoto huku akiisukuma timu zaidi mbele kwenye mashambulizi kuliko kuzuia.

Mpira wa sasa, unahitaji mabeki wa pembeni kuwa imara zaidi na nguvu za kupanda na kushuka kwa ajili ya kuisaidia timu kutoa mashambulizi ya pembeni, jambo ambalo Alonso hana.

MICHY BATSHUAYI

Ilionekana Lampard hamthamini mchezaji huyo katika kikosi chake, mashabiki wengi walikuwa wakimlaumu kocha huyo kwa kushindwa kumpa nafasi straika huyo raia wa Ubelgiji.

Hata hivyo, kwa kipindi ambacho aliaminiwa na kuanza kikosini Batshuayi alishindwa kuonesha kiwango bora, ndio maana inaaminika timu hiyo imemfungulia milango ya kuondoka katika viunga vya Stamford Bridge.

Olivier Giroud amekuwa akipewa nafasi sasa, ingawa, Lampard anafahamu kuwa staa huyo wa Ufaransa hawezi kuifikisha timu yake mahali popote zaidi ya uzoefu wake tu kikosini.

Batshuayi mwenye umri wa miaka 26, amecheza michezo 26 msimu huu na kuishia kufunga mabao sita tu. Ni mchezaji ambaye ameonesha hawezi kuibeba Chelsea.

WILLIAN

Moja ya wachezaji wanaofanya vizuri katika kikosi cha Chelsea ni Willian, ingawa, hivi karibuni ameonesha kupungua kasi, labda kutokana na umri wake wa miaka 31.

Pia, winga huyo raia wa Brazil hajaonesha dalili za kuhitaji mkataba mpya wa kuendelea kusalia Stamford Bridge, ndio maana Chelsea wamekuwa akihusishwa kuhitaji saini ya winga pindi msimu utakapomalizika.

Willian amecheza michezo 37 msimu huu, amefunga mabao saba na kutoa asisti sita. Si takwimu nzuri kwa uwezo wake ndio maana timu hiyo wanataka kumfungulia milango ya kuondoka.

Willian alikuwa mchezaji mkubwa na tegemeo wa Chelsea, lakini mwaka 2020 haukuwa mzuri kwake, hakuna kingine amabacho anaweza kuisaidia timu hiyo kwa miaka ijayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here