SHARE

NA AYOUB HINJO

WAKATI nafsi za Watanzania zikiwa na furaha ya kuiona bendera ya nchi yao ikipepea katika ardhi ya Ivory Coast, ni mwaka huo ambao staa wa Barcelona, Lionel Messi alishinda tuzo yake kubwa ya kwanza.

Miaka inaenda, muda unapita. Neymar Jr alivaa jezi ya Real Madrid kwa mara ya kwanza, alicheza mechi 48 na kufunga mabao 14. Alikuwa na umri wa miaka 17. 

Akijifua na timu ya vijana. Alizungushwa Bernabeu na kupiga picha na magwiji wa Kibrazil waliokuwa pale, Ronaldo de Lima na Roberto Carlos.

Alipohitaji kutazama mechi, Florentino Perez alimbeba hadi kwenye chumba maalumu cha VIP na kuketi naye. Neymar akaiona pepo yake akiwa hai.

Ilikuwa mwaka 2009, Tanzania ilishiriki katika michuano ya CHAN iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza. Ni ile Taifa Stars iliyokuwa chini ya Marcio Maximo aliyekesha kuwahutubia Watanzania juu ya uzalendo kwa timu yao.

Imepita miaka 10 tangu hayo matukio mawili kutokea, Taifa Stars walifanikiwa kufuzu tena CHAN inayotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Cameroon huku Messi akiweka kabatini Ballon d’Or ya sita.

Upande mwingine, yule kijana aliyekuwa na umri wa miaka 17, maisha yake hivi sasa ni kilomita 4.7 kutoka Uwanja wa Parc des Princes hadi ulipo mnara maarufu wa Eiffel, ndani ya Jiji la Paris, Ufaransa. 

Iliwahi kusemwa siku moja ‘asiyeweza kusubiri ukweli basi hawezi kusubiri kitu chochote kile duniani’. Kama unafikiri alikosea jaribu kufikiria tena.

Thamani ya ukweli ni wakati, na wakati uhitaji subira kuufikia. Subira inataka imani kuipata, ni nani mwenye imani? Ni yule mwenye kuamini. Ukisubiri na kuamini utaupata ukweli! Niliamini kwa Naseeb Abdul ‘Diamond’, nikasubiri na hatimaye ukweli umekuja.

Kwa kipindi cha miaka 10 niliyoanza kuizungumzia huko juu kuna mambo mengi yalitokea ikiwamo kwa Mwanamuziki Diamond kutoa wimbo wake wa kwanza wa Kamwambie.

Sidhani kama kuna mtu mgeni na wimbo huo, baada ya hapo zilifuata zingine nyingi Mbagala, Nitarejea, Moyo Wangu mpaka kufika kipindi hiki cha Baba lao.

Kwa sasa, Diamond ni taasisi, si Mwanamuziki wa kawaida. Anaishi katika pepo yake, sidhani kama kuna anayeweza kubisha juu ya hilo.

Katika kurasa ya mwisho iliyofunika maisha ya Mr Nice, ilianza nyingine iliyotuletea mtoto wa Tandale, mitaa iliyokosa staha ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Maisha ya Tandale hayana utofauti na bondia aliye ulingoni, unahitaji kuwa na David De Gea, Sergio Ramos,  Kevin de Bruyne, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo katika mwili mmoja ili kuyapigania maisha yako. 

Unajiokoa na kujiasisti mwenyewe. Kuna majaribu mengi sana katika mitaa hiyo, kama huamini rudi kamsikilize tena mtu yeyote aliyeishi huko.

Ndani ya Tandale, vifo na damu kumwagika ni jambo la kawaida, ubavu wako utakupa ulaji, waliodhaifu walikwenda na maji, ilihitajika uwe na moyo wa chuma kuishi maisha ya huko. 

Diamond Platnumz

Itazame dunia anayoishi Diamond sasa, shida zilizokuwa udogoni hazipo tena, ile pesa ambayo alikesha kuitafuta kwa kuuza nguo, kuruka sarakasi au kuchekesha wengine inaingia kwa urahisi tu.

Ndio, angalau Diamond aliendelea kuishi pale alipoishia Mr Nice, umaarufu kwa wakubwa mpaka watoto, hakuna ambaye hakuimba kuku kapanda baiskeli.

Mr Nice yuko wapi sasa? Sijui, kila mmoja atakuja na jibu lake, lakini ndiye alikuwa Diamond wa wakati ule, alikuwa juu ya kila mmoja kimafanikio. Amezimika ghafla kama mshumaa uliokuwa ukiwaka katika ufukwe wa bahari.

Jambo pekee ambalo naamini linaumiza kichwa na moyo wa Diamond ni hili kuhusu Tanzania, katika ardhi hii bado jasho lake halina thamani kubwa kama huko kwingineko.

Bado hana thamani hiyo anayopewa na mataifa mengine, katika mahojiano na chombo kimoja cha habari kutoka Nigeria, Mbwana Samatta aliwahi kusema “anayakumbuka maisha aliyoishi DR Congo kuliko Tanzania.”

Tofauti na inavyodhaniwa na wengi, Samatta ni mwanadamu wa kawaida sana Tanzania, hasumbuliwi licha ya kuwa maarufu labda kupigwa ‘vishoka’ na marafiki wa hapa na pale, nje ya hapo hakuna jipya juu yake.

Ndivyo ilivyo hata kwa Diamond, katika kipindi hiki ambacho ametoka kufanya shoo kwenye sherehe za ugawaji wa tuzo za Shirikisho la Soka Afrika, bado halionekani kuwa jambo kubwa Tanzania.

Wapo waliokesha mitandaoni kukosoa, wengine walikesha kufanya mambo mengine. Ilipita kirahisi tu, jaribu kuwaza kama shoo ingefanywa ya msanii kutoka Nigeria, ingekuwa furaha ya Taifa zima kila mmoja angetulia na kuangalia.

Tuache roho za chuki, Diamond alistahili kitu kikubwa zaidi kwenye safari yake ya Misri.

Jibu ni rahisi sana, mpaka leo Watanzania wamegoma kuiona thamani ya sauti ya Diamond kwa taifa hili. Wamegoma kuiona tofauti ya muziki wetu miaka 10 iliyopita na ilivyo sasa.

Achana na Bongo Fleva, chukua aina zote za muziki zilizokuwa zikipigwa nchini. Rhumba, taarab, dansi, mduara na mchiriku, lini muziki wetu uliwahi kuwa namba moja Afrika?

Unafikiri kulikuwa na wasanii wa kawaida? Hapana, kulikuwa na vipaji vya kila aina hapa lakini kilicholeta tofauti ya muziki wa nyakati zile na hizi ni Diamond Platinumz, huu ndio ukweli mchungu ambao wengi tumegoma kuumeza!

Ni Diamond aliyeufanya muziki wetu kuwa namba moja Afrika, ni yeye aliyefanya wasanii wetu kuheshimika nje ya mipaka ya Taifa letu.

Diamond Platnumz akiwa na Mpenzi wake Tanasha Donna

Afrika hii, ni nani asiyemfahamu Diamond? Sidhani kama yupo, si Davido wala Wizkid wote wanalitaja jina lake kwa adabu. Rick Ross hata wengine wa huko majuu wanamfahamu.

Huenda mpaka anaimaliza pumzi yake ya mwisho duniani, TX Moshi William hakuwa na umaarufu kama alionao Harmonize au Rayvan leo hii nje ya mipaka ya Tanzania.

Miaka 10 ya Diamond katika muziki, yamekuja na mabadiliko makubwa kwenye tasnia hiyo, sasa hakuna msanii anayeweza kutoa video ya wimbo ambayo haina ubora na ubunifu. Yote hayo, kuangalia kama itaweza kupenya anga za kimataifa.

Diamond Platnumz

Kila msanii ukimuuliza ana malengo gani na muziki wake, majibu hayawezi kutofauti zaidi ya kutaka mafanikio na kuufikisha mbali zaidi muziki wa Tanzania.

Diamond ni sehemu kubwa ya mafanikio kwa Wanamuziki wengine ndani ya nchi hii, kuanzia malipo ya shoo mpaka uwekezaji mkubwa wa fedha kwenye kazi zao.

Ni ngumu kulitaja jina lake kwa sasa, lakini Diamond akae akijua hata asali huonjwa kwa ncha ya kisu. Utamu na maumivu, kila kitu huja kwa wakati wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here