SHARE

NA NIHZRATH NTANI

USIKU wa leo Jumatano, Septemba 28, macho na masikio ya wapenda soka ulimwenguni kote yataelekezwa jijini Madrid, nchini Hispania, katika dimba la Vicente Calderon, uliopo Wilaya ya Arganzuela.

Kwa mujibu wa vipimo, Vicente Calderon ni uwanja unaotajwa kuwa ni mkubwa katika sehemu ya kuchezea, ukiwa na urefu wa mita 105 na upana mita 70. Ni mkubwa kuliko viwanja maarufu kama Allianz Arena, Old Trafford, Nou Camp, Anfield na hata Santiago Bernabeu.

Usiku wa leo, nyasi za uwanja huo zitawaka moto, wakati miili ya wanaume 22 itakapokuwa inapambana katika mechi inayochukuliwa kuwa itakuwa yenye kusisimua mno.

NI MECHI YA KULIPA KISASI?

Timu yoyote itakayoibuka mshindi usiku wa leo kati ya Atletico au Bayern Munich itakuwa imelipa kisasi kwa namna fulani.
Carlo Ancelotti na Diego Simeone wamekutana mara 13 ndani ya miaka mitatu iliyopita, huku Diego Simeone akiibuka na ushindi katika mechi tano, wakati mechi nne akipoteza dhidi ya Carlo Ancelotti na mechi nne wakitoshana nguvu.

Carlo Ancelotti aliweza kumfunga Diego Simeone katika michuano ya Copa del Rey hatua ya nusu fainali, akiibuka mshindi nyumbani na ugenini katika msimu wa 2013/2014. Pia Carlo Ancelotti aliibuka mshindi katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kule Lisbon -Ureno.

Vile vile aliweza kumwondoa Diego Simeone msimu wa 2014/2015 katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa goli la ‘Chicharito’, baada ya kutoa sare katika mechi ya kwanza. Hata hivyo, Ancelotti hakuwahi kumfunga Diego Simeone katika mechi yoyote ya La Liga, mpaka anatimuliwa Real Madrid mwaka 2015.

Ni msimu uliopita tu wakati Diego Simeone alipoweza kuiongoza Atletico Madrid kuiondoa Bayern Munich, iliyokuwa chini ya Pep Guardiola katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa hiyo, mechi hii ya hatua ya makundi inaweza kuchukuliwa kama kisasi kwa makocha wote wawili. Ushindi wa Bayern dhidi ya Atletico utakuwa na maana kubwa kwao na kocha wake, Ancelotti kwa sababu ya kuonekana ana takwimu mbovu dhidi ya Diego Simeone wanapokutana.
Na ushindi wa Atletico Madrid utakuwa na maana nyingine ya kuendeleza ubabe wake kwa Bayern na pia kulipa kisasi kwa Carlo Ancelotti kwa kipigo walichokipata mara ya mwisho Aprili 22, 2015, wakati huo Ancelotti akiwa kocha wa Real Madrid.

ANTOINE GRIEZMANN VS ROBERT LEWANDOWSKI

Mioyo ya mashabiki wa kila timu usiku huu itaelekezwa kwa watu hawa wawili. Wanaume hawa wawili wameibuka kuwa washambuliaji hatari mno msimu huu, mpaka sasa Antoine Griezmann akiwa amefunga magoli 5 katika mechi 6 alizocheza kwa mashindano yote, wakati mpinzani wake, Robert Lewandowski akiwa ameshatupia magoli 6 katika mechi 6 za mashindano yote msimu huu. Kosa moja la mabeki wanaweza kukuadhibu.

VITA YA SEHEMU YA KIUNGO.

Sifa kubwa ya Atletico ni kuwa na wachezaji wengi mahiri na wenye nguvu katika sehemu ya kiungo. Kama uliweza kuwatazama vyema katika mechi yao ya sare dhidi ya Barcelona, unaweza kukubaliana nami. Katika mfumo wa 4-2-3-1 anaopenda kuutumia Diego Simeone mara nyingi umepelekea kutawala sana sehemu ya kiungo.

Hata hivyo, usiku wa leo Atletico Madrid inakutana na Bayern Munich mpya kabisa. Carlo Ancelotti ni muumini wa mfumo wa 4-3-3, akitumia sana viungo watatu madhubuti kati.
Kazi kubwa leo itakuwa kati ya Yannick Carrasco, Saul Niguez, Koke, Nico Gaitan, Angel Correa dhidi ya wale wa Bayern akina Alonso, Artulo Vidal, Joshua Kimmich, Thiago Acantara, Renato Sanchez na Frank Ribery. Hakika ni jasho na damu usiku huu.

HAWA WATAKOSEKANA

Atletico Madrid watawakosa wachezaji wake wawili muhimu mno usiku huu, akiwemo kiungo wake bora, Augusto Fernandez, pia itawakosa beki wake Jose Gimenez, kiungo mkongwe Tiago Mendez, Alessio Cerci na kipa wake, Angel Moya, walio majeruhi.

Bayern Munich wao hawatakuwa na pengo kubwa pamoja na kuwakosa Douglas Costa na Holgar Badstuber, huku kukiwa na hatihati kumkosa beki wake mahiri, Mats Hummels, walio majeruhi.

TIMU IPI ITAIBUKA NA USHINDI?

Kiwango cha Bayern Munich msimu huu kinatisha. Wamecheza mechi sita na kushinda zote. Chini ya Carlo Ancelotti Bayern taratibu wanaanza kurejea katika aina ya asili ya soka lao la kasi na pasi ndefu za haraka haraka.

Ni wazuri pia kwa mipira ya kushtukiza, huku wakiwa na wachezaji wenye uwezo wa kupiga mashuti hata nje ya 18. Ni hatari zaidi kwa mipira ya kona na krosi.

Msimu huu wameimarika mno, tofauti na msimu uliopita. Kurejea kikosi cha kwanza kwa Javi Martinez na kuwasili kwa Mats Hummels na Renato Sanchez na kuibuka kwa kinda Joshua Kimmich kumewafanya Bayern Munich wawe imara zaidi kuliko msimu uliopita.

Atletico Madrid hawajaanza vyema msimu huu wakiwa wamecheza mechi saba, huku wakitoa sare mechi mbili na kushinda tano. Msimu huu Atletico Madrid ni moja ya timu zilizofanya vyema katika dirisha la usajili kwa kuwatwaa wachezaji bora na mahiri kama Nico Gaitan na Kelvin Gameiro.

Ni imara sana katika sehemu ya kiungo na ushambuliaji, huku sehemu ya ulinzi nako kukiwa na wanaume wa shoka kweli kweli. Atletico Madrid wakiwa nyumbani kwao Vicente Calderon wanakuwa timu tofauti. Ni ngumu mno kuwafunga nyumbani kwao.

Mshindi wa mechi hii atakuwa amejiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na nafasi kubwa ya kuongoza kundi hili ‘D’ kwa hatua inayofuata. Ni mechi kubwa na bora kuitazama usiku huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here