SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

KASI ya zao la mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba, Miraji Athuman ‘Sheva’, imekuwa tishio kwa wapinzani kutokana na uwezo wake ambao ameuonyesha katika mechi nne zilizopita za mikikiki hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Miraji alifanikiwa kuendelea kuwa chachu kwa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi baada ya kufunga bao matata akimalizia mpira mrefu uliochongwa na Ibrahim Ajib katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United.

Baada ya mchezo huo, Miraji aliliambia DIMBA Jumatano kuwa ni jambo jema kufananishwa na straika wa zamani Simba, Emmauel Okwi, akiamini anahitaji kuvaa viatu vyake.

Kauli hiyo ilifuatia kelele za mashabiki waliokuwa wakimtaja Miraji kama Okwi mpya ndani ya kikosi cha Simba.

“Okwi ana heshima yake kuanza kunifananisha naye kwa sasa bado ila naona hii ni baraka kwangu kwa sababu nami nataka nifikie kiwango kile waendelee kunipa moyo tu,” alisema.

Miraji hadi sasa amefungia Simba mabao matatu, huku akitoa ‘assist’ mbili yaani katika mabao 10 ya timu nzima yeye na Meddie Kagere wamehusika kwa asilimia 100.

Winga huyo aliyepitia Toto African, Mwadui na Lipuli, alianza msimu kwa kishindo baada ya kufunga mchezo wa kwanza dhidi ya JKT Tanzania katika ushindi wa mabao 3-1.

Akawatungua Mtibwa Sugar katika mchezo uliofuata na baadaye akasababisha mkwaju wa penalti dhidi ya Kagera Sugar, ikawekwa kambani na Kagere.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here