SHARE

NA SAADA SALIM,

EMMANUEL Okwi anahesabu siku tu kutua Simba na tayari ameanza mipango ya maisha yake mapya ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi kwa kukamilisha dili la kusaini mkataba wa miaka miwili.

DIMBA lina taarifa zisizo na shaka kuwa straika huyo Mganda, alitumiwa ujumbe wa fax ukiwa na vipengele vya mkataba na baada ya kuusoma ameridhia kila kitu kilichomo.

Na sasa anachokifanya ni kuanza kuamshawishi winga kipenzi cha mashabiki, Shiza Kichuya, waongee dili la kumwachia jezi yake namba 25 ambayo alikuwa akiitumia.

Okwi amekiri kwamba amekuwa akifuatilia sana viwango vya wachezaji wa Simba na amekubali uwezo wa Kichuya pamoja na anachofanya uwanjani na kwamba yeye akitua wakiungana moto utawaka.

Kwa sasa Okwi amemaliza mkataba wa kuichezea klabu ya SC Villa ya Uganda, ambayo ndiyo iliyomkuza kisoka baada ya kuvunja mkataba huko Denmark alikokuwa anasugua benchi. Kilichobaki ni kwamba anasubiri tu kurejea Simba msimu ujao na tayari ameshaafikiana mambo mengi na viongozi na atatua muda wowote benchi la ufundi linaloongozwa na Joseph Omog litakapotaja tarehe rasmi ya kuanza msimu mpya.

Mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wana hamu kubwa ya kumuona mchezaji wao huyo anawasili na kutumikia kikosi cha timu hiyo kwa mara nyingine hasa kipindi hiki Simba itakapokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).

DIMBA lilipata taarifa za uhakika ndani ya klabu hiyo kwamba  mchezaji huyo ameingia makubaliano na Simba ya miaka miwili na kuanzia sasa atatua nchini kukamilisha taratibu zote za usajili.

Alisema utaratibu wote umefanyika baada ya mchezaji huyo kuridhia makubaliano hayo na kipindi cha sikukuu familia yake ilikuja nchini kwa ajili ya mapumziko mafupi.

“Suala la Okwi kwa sasa halina mjadala, kwani klabu ya SC Villa aliyokuwa akiichezea amekwishamalizana nayo kabisa baada ya kusaini mkataba wa muda mfupi kwa ajili ya kulinda kiwango chake na alipata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo ndio ilikuwa silaha yake ya kwanza ili kutua Simba msimu ujao,” chanzo cha habari kutoka Simba kililiambia DIMBA.

Okwi kwa hivi sasa yumo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda iliyokwenda nchini Addis Ababa kuvaana na timu ya Taifa ya nchi hiyo.

Straika huyo pamoja na beki wa Kimataifa wa Uganda na klabu ya Simba, Juuko Murshid, wote kwa pamoja wamejumuishwa katika kikosi cha mwisho cha timu ya Taifa ya Uganda.

Mtoa habari huyo alisema usajili wa Okwi utaongeza makali ya safu ya ushambuliaji baada ya uwepo wa Laudit Mavugo, Kichuya pamoja na John Bocco aliyesajiliwa msimu huu.

Mbali na Okwi na John Bocco, pia kipa wa Azam FC, Aishi Manula, anasemekana kumwaga wino kwa Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kubakiza mwezi mmoja katika mkataba wake na klabu yake, huku akigoma kuongeza mwingine.

3 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here