SHARE

MANCHESTER, England

ULIKUWA ni mchezo uliohitaji maamuzi sahihi na katika hili, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, alifanikiwa kuepukana na kichapo kingine kutoka kwa Jose Mourinho wa Manchester United, baada ya kufanya mabadiliko yaliyozaa bao la kusawazisha, lililobadili matokeo katika dakika za lala salama za mtanange huo.

Arsenal ilisafiri hadi jijini Manchester kuvaana na wapinzani wao hao kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, uliopigwa jana jioni, ambapo miamba hao walitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.

Manchester United ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kiungo Juan Mata, aliyetumia vizuri pasi ya Ander Herrera na kuutumbukiza mpira wavuni katika dakika ya 69 ya mchezo.

Zikiwa zimesalia dakika 25 mpira kumalizika, Wenger alifanya mabadiliko ya kuwatoa wachezaji watatu, Mohamed Elneny, Francis Coquelin na Carl Jenkison na kuwaingiza Olivier Giroud, Alex Oxlade Chamberlain na Granit Xhaka.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda, kwani ndani ya dakika nne za nyongeza, Arsenal walifanikiwa kusawazisha bao hilo baada ya Giroud kuruka juu na kuunganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliochongwa na winga Chamberlain.

Bao hilo la dakika za lala salama limewasaidia Arsenal kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi yoyote kati ya 17 za michuano yote msimu huu, ingawa bado haijafanikiwa kumfunga Mourinho katika michezo 12 ya ligi, huku kikosi chake kikimaliza mchezo na shuti moja tu lililolenga goli jana.

Hata hivyo, matokeo hayo yanaendelea kuiweka United kwenye mazingira magumu hivi sasa, kwani wamekusanya pointi tano tu kwenye michezo yao mitano ya mwisho kwenye ligi ndani ya dimba lao la Old Trafford.

Mourinho alimwanzisha mshambuliaji Marcus Rashford kwenye nafasi ya Zlatan Ibrahimovic, anayetumikia adhabu na kumwacha nahodha Wayne Rooney kwenye benchi.

Mmoja wa wachezaji ambao hawakutegemewa kuanza ni Antonio Valencia, ambaye alitoka kuumia mkono na alianzishwa kama beki wa kulia, nafasi aliyocheza Ashley Young kwenye mchezo dhidi ya Swansea City.

Habari kubwa kwa upande wa Arsenal ilikuwa ni kumhusu mshambuliaji Alexis Sanchez, aliyepata maumivu ya msuli wa paja alipokuwa akiitumikia timu ya taifa ya Chile na kulikuwa na hofu iwapo ataanzishwa kwenye mchezo dhidi ya United.

Beki Carl Jenkinson alianzishwa kwenye upande wa kulia, akichukua jukumu la Hector Bellerin, aliye majeruhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here