SHARE

NA JESSCA NANGAWE

YANGA hawataki masihara.Uongozi wa klabu hiyo na wadhamini wao kampuni ya GSM wameamua kuweka pembeni maumivu ya kichapo cha mabao 4-1 walichokipata kutoka kwa watani zao wa jadi Simba na sasa wameingia rasmi sokoni kusaka majembe ya nguvu kwa ajili ya kukisuka upya kikosi cha timu hiyo.

Kichapo ilichokipata Yanga ni kama sasa kimewazindua mabosi wa GSM,uongozi na benchi la ufundi kuona hawatakiwi kupoteza muda kufanya usajili kwani matokeo ya mechi hiyo yameonyesha namna kikosi chao kilivyo ‘nyanya’ katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa ambazo DIMBA Jumatano imezipata kutoka ndani ya Yanga zinaeleza,Kocha Luc Eymael, ametakiwa kuwasilisha fasta ripoti yake ili akabidhiwe fungu la usajili wa nguvu utakaoendana na kasi ya mabadiliko ya mfumo wa uongozi ambayo GSM inasimamia mchakato wake.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Injinia Hersi Said, amenukuliwa na chanzo chetu akisema mechi na Simba imewashtua na kuwadhehesha wao kama wadhamini na sasa wanataka kuona Yanga inasukwa upya ili kujibu mapigo ya ubora walionao wapinzani wao.

“Kocha ameambiwa awasilishe ripoti yake haraka kwani wadhamini wameumizwa na matokeo ya aibu timu iliyopata na sasa wanataka benchi la ufundi liingie sokoni haraka kutafuta nyota wa kimataifa na wazawa wenye viwango vikubwa vitakavyoendana na Yanga ijayo,”alinukuliwa mtoa taarifa.

ìMoja ya mipango yetu ni kuona Yanga mpya inaundwa kwa lengo la kurejesha furaha ya mashabiki wetu hilo tutalifanikisha kwa kufanya usajili mzuri sambamba na kuleta mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji timuîalisema Said.

DIMBA lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo,Frederick Mwakalebela, mikakati yao ambapo,alisema,watafanya usajili wa kishindo na tayari mchakato huo umeanza huku wakiwa na majina matano ya wachezaji wa kigeni na manne ya wachezaji wazawa.

ìMipango yetu kwa sasa ni kumaliza Ligi vyema, tunataka kushinda michezo yote iliyosalia, pili tulishaanza mipango ya kuboresha timu na wapo wachezaji watano wa kimataifa na wanne hapa nyumbani ambao tutakwenda kuwaongeza ndani ya kikosi chetuîalisema Mwakalebela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here